Bongo Fc


Makala: hili la simba na yanga sasa limekuwa sugu

Na: Omary Ramsey
Email: omaryramsey@gmail.com

Ni siku nyingine tunakutana katika makala za soka kutoka BongoFC pekee, kumbuka makala hizi ni kila siku ya Jumanne na Alhamisi.

HERE WE GO... Timu zote 16 zinazocheza michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara mpaka sasa zimeshacheza michezo sita, huku mahasimu wa soka Simba na Yanga zikiendeleza ufalme wa miaka mingi kwa kukaa juu katika msimamo wa ligi hiyo.

Kwa nyakati tofauti timu hizo zimekuwa zikibadilishana kukaa kileleni, ambapo wiki iliyopita Yanga iliongoza msimamo huo Simba nayo ikawaondoa kileleni baada ya kucheza mechi yake iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar na kukwea tena kileleni, licha ya timu zote hizo kuwa na pointi 12 sawa sambamba na timu za Azam FC na Mtibwa.

Ushindani huo kwa kiasi kikubwa umeongeza msisimko katika michuano hiyo mwaka huu, kiasi cha mashabiki na wadau wa timu hizo kila mmoja kutamani kuiona timu yake ikiongoza.

Ghafla upepo huo umegeuka, sasa kinachojadiliwa ni mechi ya vigogo hao wa soka Simba na Yanga wanaotarajia kuumana Oktoba 28 mwaka huu.Hakuna tena mijadala mizuri iliyokuwa ikiendeshwa kama vile uchambuzi wa baadhi ya wachezaji pamoja na mikakati mingine ya ushindi, bali kinachozungumzwa zaidi ni juu ya mechi hiyo kwamba kila mmoja ataibuka na ushindi dhidi ya mwingine.

Mara nyingi inapokuja mijadala inayohusu mechi ya watani hao wa jadi, hakuna uchambuzi wa kiufundi unaozungumza kama vile upangaji timu au jinsi mchezaji fulani anavyoweza kucheza vizuri akipangwa na fulani, bali kinachoendelea ni ubishi tu na mambo mengi yasiyokuwa na tija katika soka la Tanzania.

Mbaya zaidi ni pale wadau wa timu hizo wanavyohangaika kuhakikisha timu zinapata kambi zilizojificha kwa ajili ya maandalizi, lakini ukiuliza kwa undani sababu za kujificha huko sababu itakayotolewa itakuwa ni kukwepa fitina au mambo ya kishirikina.

Sisi BongoFC tunaona kwamba aina hii ya ushabiki kamwe haina tija katika soka letu, na pengine ndiyo huu unaolisababishia kandanda la Tanzania kuendelea kushuka katika viwango vya Fifa kila kukicha.Mienendo yetu isiyobadilika na kutupeleka katika misimamo ya kisayansi, unatusababishia tutembee njia tofauti na wenzetu wanaotafuta maendeleo ya kweli ya soka lao.

Tunaonekana kana kwamba sisi tunahesabu makuti ilihali wenzetu wanahesabu nazi, jambo ambalo kwetu haliwezi kutuletea faida asilani.

BongoFC tunatamani sasa wadau wachoke kuona ushindi mtamu kwao ni ule wa Simba au Yanga kushinda, bali wafikirie lini mchezaji kutoka katika klabu hizo atanunuliwa kwa bei kubwa kwenda kucheza soka la kulipwa nje.

Tuone fahari kwetu pale tutakapokuwa na timu ya Taifa iliyojaa wachezaji wanaocheza soka la kulipwa, kwani hiyo ndiyo njia waliyoitumia wenzetu waliofanikiwa katika mchezo huo na kutuacha sisi tukihesabu miaka 70 ya kuwepo timu zetu bila kuwa na manufaa yoyote.

Tunafahamu kwamba Simba na Yanga hazitaacha kuwa na ushabiki uliopindukia, kwani hiyo ni fahari yake kutokana na historia iliyokuwepo nchini, lakini pamoja na yote hayo hivi ni kweli tunahitaji kuona juhudi zile zilizofanywa na wahenga waliozianzisha ndiyo zinaishia pale?

Tujiulize tu kama wazee hao waliweza kujenga hadi nyumba za ghorofa kwa uchache wao na kutokuwepo kwa teknolojia yoyote ya kusukuma maendelo, hivi sisi tumefanya nini kuendeleza pale walipoishia. Tutafakari kisha tuone fahari ya kulisukuma soka leo kuelekea katika maendeleo ya kweli.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.