Bongo Fc


Asikwambie mtu mavugo anapendwa simba!

Kama ulidhani mashabiki wa Simba wamemsahau mshambuliaji wao wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo, kutokana na ujio wa John Bocco, unajidanganya kwani straika huyo amedhihirisha bado ni kipenzi cha mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi hao.

Mavugo alionyesha ubora wa hali juu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara juzi dhidi ya Njombe Mji uliopigwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Simba kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0.

Kiwango kilichoonyeshwa na mchana nyavu huyo kilisababisha jina lake kuimbwa mara kwa mara na mashabiki wa timu hiyo waliopagawa na uwezo wake, huku wengine wakisema kuwa Bocco anapaswa kuwa makini mbele ya mkali huyo.

Mashabiki waliojitokeza katika mchezo huo walikuwa wakiimba ‘King King King Laudit’, huku wakisifia uwezo wa mshambuliaji huyo ambaye hadi sasa amepachika mabao mawili katika michezo mitatu aliyoshuka dimbani, wakati Bocco akiwa amefunga bao moja tu.

Mavugo ambaye alicheza kama mshambuliaji wa mwisho katika mchezo huo, alikuwa akisaidiana na Emmanuel Okwi ambaye pia alipachika bao moja katika ushindi huo mnono.

Mrundi huyo alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Njombe Mji iliyokuwa chini ya nahodha, Laban Kambole pamoja na Ahmed Adiwale ambao mara kwa mara walikuwa wakimfanyia madhambi mchana nyavu huyo.

Mavugo ameandika bao lake la pili msimu huu, huku akianza kwa mara ya kwanza katika kikosi cha Joseph Omog baada ya kupoteza namba mbele ya Bocco.

Licha ya kuonyesha kiwango cha hali ya juu, mshambuliaji huyo hakumaliza dakika 90 kwani alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mshambuliaji raia wa Ghana, Nicholas Gyan.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.