Bongo Fc


Ni lini mpira wetu utaenda mtandaoni?

Na: Omary Ramsey

Dunia imekuwa kijiji. Siku hizi unaweza ukampata mwanamke mtandaoni, mkapendana, mkaelewana, mkagombana na mpaka mkaachana bila hata kuonana. Cha msingi ni kuendelea kuwa na bando tu.

Unaweza ukawa unaishi Tanzania lakini ukawa kila siku unatazama mpira wa nje, muvi za nje, siasa za nje na hata muziki wa nje. Tuko kwenye dunia ambayo biashara ya mtandaoni haiepukiki. Ni muda wa kuupeleka sasa mpira wetu mtandaoni.

Ligi Kuu Tanzania inapaswa kupelekwa mtandaoni. Hakuna namna, takwimu na rekodi mbalimbali za timu zetu na wachezaji ni muda wa kuziweka wazi mtandaoni. Usajili na mishara ya makocha na wachezaji lazima iwekwe wazi mtandaoni ili kuondoa utata ambao umekuwa unarudisha nyuma maendeleo ya mpira wetu. Kila kitu kwenye dunia ya leo kinapatikana mtandaoni, hata ukitaka mke au muwe ni rahisi tu.

Clement Sanga siku chache zilizopita alishinda uchaguzi na kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hongera sana kwake. Natarajia kumwona Sanga akiwa mstari wa mbele katika kuziongezea kipato klabu zetu.

Njia moja wapo ni kutumia mtandao. Ligi zetu Tanzania zinatakiwa kuonekana dunia nzima kupitia mtandao. Huu ni wakati wa Clement Sanga na watendaji wake kufanya tafiti na kuona ni namna gani Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuanzia inavyoweza kuonekana mtandaoni.

Haki za matangazo ya ligi yetu mtandaoni, itachangia pia kuongeza kipato kwa klabu zetu na kupata mashabiki wengi nje ya nchi. Dunia imebadilika ni lazima na sisi tubadilike. Mpira wetu ni lazima uende mtandaoni na mtu pekee wa kusimamia hili ni mwenyekiti wa Bodi ya Ligi ambaye kimsingi ndiye mtetezi wa klabu zote zinazosimamiwa na Bodi hiyo.

Clement Sanga akilisimamia hili kwa uadilifu litamjengea sifa na hali ya kuaminika zaidi, kwa sababu watu wengi ndani na nje ya nchi watapata fursa ya kuitazama ligi yetu. Tunahitaji kuona Bodi ya Ligi inayoendeshwa kisasa.

Takwimu zote za wachezaji na klabu ziwekwe kwenye website ya Bodi na iwe rahisi kwa mtu yeyote kuweza kuona. Tunaweza kuvutia pia watu wengi nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye mpira wetu. Tusiendelee kujifungia kwenye boksi wakati dunia inazidi kuwa kijiji.

Tunatakiwa tupate “Live streaming” za mpira wetu. Msimu ujao kuna timu sita kutoka daraja la kwanza ambazo zitapanda daraja na kuja Ligi Kuu, huu ni muda muhimu sana wa kutupia jicho katika ligi hiyo. Tusipokuwa makini, tutaongea idadi tu na usio ubora kwa timu zinazopanda daraja na kwa bahati mbaya, mechi zote hazionyeshwi na kituo chochote cha televisheni wala mitandaoni.

Mitandao inasaidia sana kuwafikia watu wengi kwa wakati, Bodi ya Ligi wasitolee tu macho Ligi Kuu. Wanapaswa kutazama upande mwingine na kujenga ushawishi. Kuna haja ya kuinua msisimko wa ligi za madaraja ya chini ambayo kimsingi ndiyo yanapaswa kuwa “Mama” wa Mpira wa Tanzania.

Bodi ya ligi ni lazima iwe na kitengo kilichokamilika cha dijitali kinachoweza kwenda na kasi ya dunia hii. Klabu pia hazitakiwi kulala katika hili, kuna fedha nyingi sana kupitia biashara ya mtandaoni kwenye Soka.

Tunahitaji kubadilika ili tuendane na kasi ya ulimwengu huu. Mpira wetu ukianza kuonyeshwa mtandaoni, tutatengeneza fedha nyingi sana na pia kujiongezea mashabiki dunia nzima. Hizi zinapaswa kuwa ni kazi za awali kabisa za mwenyekiti mpya wa Bodi ya Ligi, kaka yangu Clement Sanga.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.