Bongo Fc


Yanga vs simba.. ugali moto, mboga moto!

Kutokana na viwango vya soka vilivyoonyeshwa na Yanga, Simba kwenye mechi zao mwishoni mwa wiki iliyopita pamoja na takwimu walizokusanya baada ya mechi saba za Ligi Kuu Tanzania Bara, inatoa picha halisi ya upinzani utakaokuwapo kwenye mtanange wa watani hao wa jadi utakaopigwa Jumamosi hii.

Kwa sasa Simba ambao ni vinara wa Ligi Kuu Tanzania, wako moto na Yanga wanaoshika nafasi ya pili pia ni moto, ambapo kwa watoto wa mjini wanasema ugali moto na mboga moto.

Mpaka sasa mechi hiyo haijajulikana itachezwa wapi, ingawa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeonyesha kuwa mchezo huo unaweza kupigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Lakini kutokana na mchezo huo wa Yanga na Simba kuwa ni moja ya ‘derby’ kubwa barani Afrika, ukiziacha zile za Orlando Pirates na Kaizer Chiefs (Afrika Kusini), Raja Casablanca vs Wydad Athletic Club (Morocco), Al Ahly vs Zamalek (Misri), Club Africain vs Esperance Sportive de Tunis (Tunisia), bila shaka Serikali inaweza kubadili maamuzi hayo na mchezo huo kuhamishiwa Uwanja wa Taifa.

Ikiwa ni mara ya pili mahasimu hao kukutana msimu huu, baada ya ule mchezo wa Ngao ya Jamii kwa ajili ya kufungua pazia la Ligi Kuu ambao ulimalizika kwa sare ya 0-0 na Simba kubeba taji hilo kwa matuta 5-3.

Katika mchezo wa mwisho, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Njombe Mji, kabla ya Yanga kujibu mapigo kwa kuichapa Stand United 4-0.

Matokeo hayo yamefanya timu hizo ambazo zimeshinda mechi nne na kutoka sare tatu, kufikisha pointi 15 kila moja lakini Simba wakikaa kileleni kwa idadi kubwa ya mabao ya kufunga, ambayo ni 19 wakati Yanga wakitingisha nyavu mara 10 pekee.

Mchezo huo utatoa picha ya ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na upinzani uliopo, kwani atakayeshinda atakuwa atamwacha mwenzake kwa pengo la pointi tatu, ingawa watakuwa na kazi kubwa kutokana na kufukuziwa kwa karibu na Mtibwa Sugar ambayo pia ina pointi 15, huku kiwango chao msimu huu kikiwa juu.

NI MECHI YA AJIB NA OKWI

Kwa kiasi kikubwa mchezo utatawaliwa na majina ya washambuliaji Emmanuel Okwi ‘Mhenga’ wa Simba na Ibrahim Ajib (Yanga), ambao wameonekana kuwa moto wa kuotea mbali kwenye upachikaji wa mabao msimu huu.

Okwi ambaye amerejea Simba msimu huu akitokea Sports Villa ya Uganda, tayari ameshacheka na nyavu mara nane ikiwamo ‘hat-trick’ aliyopiga dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi walioshinda 7-0.

Naye Ajib ambaye alijiunga Yanga msimu huu akitokea Simba, ameshapachika mabao matano, yakiwamo mabao yake mawili ya mpira wa adhabu ambayo yamekuwa gumzo kwa mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani.

Pamoja na takwimu hizo za mabao kwa upande wa Okwi, lakini nyota huyo amekuwa akifanya vizuri kwenye mechi hizo za watani wa jadi ambapo mabao yake mawili aliyofunga wakati Wekundu wa Msimbazi wanaichapa Yanga 5-0 mwaka 2012, yamebakia kumbukumbu kwenye vichwa vya mashabiki wa soka nchini.

Lakini hiyo imekuwa tofauti kwa Ajib ambaye alishindwa kutamba kabisa kwenye mechi hizo akiwa Simba, ambapo kwenye mechi yake ya kwanza ambayo ilikuwa ni ya Ngao ya Jamii, pamoja na kumaliza mchezo huo lakini hakuonyesha makali yoyote.

Lakini mechi hii inawezekana ikawa tofauti kwa Ajib na akafanya maajabu na kuibeba Yanga kutokana na kasi yake ya kupachika mabao, huku uzoefu wa Okwi na kiwango anachoonyesha inaonyesha wazi kwamba mechi hiyo itakuwa ya aina yake kwao na lolote linaweza kutokea.

VITA YA TSHISHIMBI NA MKUDE

Pamoja na safu ya washambuliaji ya timu hizo kupewa nafasi kubwa ya kung’ara kwenye mechi hiyo, lakini utamu wa mchezo huo utakuwa kwenye safu ya kiungo kutokana na kila mmoja kuwa na wachezaji imara.

Yanga wanamtegemea kiungo wao wa DR Congo, Papy Kabamba Tshishimbi, ambaye tangu ametua msimu huu ameonyesha uwezo mkubwa na kukifanya kikosi hicho kuwa na uhai kwenye safu ya kiungo.

Uwezo wa kiungo wa Simba, Jonas Mkude, unafahamika na mashabiki wa soka nchini ingawa wawili hao hawatakutana moja kwa moja kutokana na kila mmoja kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, lakini wanaweza kukumbana kwenye eneo hilo na kutakuwa na shughuli pevu.

Mashabiki wa soka nchini wamekwishaanza kujadili mchezo huo kwa upande huo wa kiungo, kutokana na Mkude kurejea kwenye kikosi cha kwanza cha Simba baada ya kuwekwa benchi mechi kadhaa, huku

Tshishimbi akiendelea kuwateka mashabiki wa Yanga tangu atue nchini akitokea akitokea Mbambane Swallows ya Swaziland.

HATIMA YA MAKOCHA

Mara kwa mara Yanga na Simba zinapokutana makocha ndio wanaoangushiwa jumba bovu pale inapotokea timu mojawapo imepoteza mchezo huo wa watani wa jadi.

Kocha wa Cameroon anayekinoa kikosi cha Joseph Omog na mwenzake anayeinoa Yanga, George Lwandamina wa Zambia, wote wanaonekana kukalia kuti kavu kutokana na mwenendo wa vikosi vyao, ingawa bado timu ziko kwenye nafasi mbili za juu ila mashabiki hao hawavutiwi na soka linaloonyeshwa.

Licha ya Omog kuisaidia Simba kurejea kwenye michuano ya kimataifa tangu mwaka 2012, lakini amekuwa akionekana hana uwezo wa kukinoa kikosi hicho kilichosheheni wachezaji nyota ambacho kilipaswa kishinde mechi zote ambazo wametoka sare dhidi ya Azam FC, Mbao FC na Mtibwa Sugar.

Hali hiyo inayomkumba Omog inaendana na ile ya Lwandamina, ambaye anaonekana hafai baada ya kutoka sare na Lipuli iliyopanda daraja msimu huu, kabla ya kutoka sare nyingine na Majimaji kisha na Mtibwa.

Hivyo matokeo mabaya kwa upande wowote kwa timu hizo yanaweza yakasababisha kocha mmojawapo kufungashiwa virago vyake.

MANULA NA ROSTAND

Mchuano mwingine utakuwa kwa makipa wa timu hizo, Youthe Rostand wa Yanga na Aishi Manula ambao kwenye Ngao ya Jamii walipokutana Agosti 26, mwaka huu hakuna aliyeruhusu bao.

Tangu msimu huu uanze, Rostand ameruhusu mabao mawili, huku Manula akiruhusu manne na kuonyesha wazi mchezo huo utakuwa na upinzani mkubwa kila idara.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.