Bongo Fc


Moto wa valverde mnauona lakini?

Na: Omary Ramsey

NI mapema sana kumtaja bingwa wa michuano ya Champions League mwaka huu. Kuna timu zinazoonekana kweli zimepania kufanya maajabu na kweli zinapania hata ukiwatazama kwenye mechi zao utagundua hilo.

Lakini nani anayeiwaza Barcelona kwa sasa? Wachache sana. Nini kimesababisha hili? Kuondoka kwa Neymar? Ujio wa kocha ambaye anajulikana na wachache?

Wengi wanaonekana kuvutiwa na PSG. Pia wamezidi kuisahau Barcelona baada ya Jupp Heyckens kurudi Bayern Munich. Maisha ya hizo timu mbili aidha Man City au Man United, yameipoteza Barcelona kwenye midomo ya watu.

Lakini kuna ukweli unaotakiwa kusemwa juu ya huyo kocha mpya, Valverde. Na itabidi ieleweke tu.

Ni dhambi kutoitaja Barcelona ya Valverde katika orodha ya timu zenye uwezekano wa kutwaa taji la Champions League mwaka huu, kwanini? Vijana wake wanaonekana ‘kukomaa kwa vita’ kila baada ya wiki.

Turahisishe mambo hapa, tukiziangalia takwimu za Barca, kila kitu kinaonekana kuwanyookea msimu huu. Wameshinda mechi zote tatu za awali kwenye Champions League kwa mara ya kwanza kabisa.

Waliomtangulia ilikuwaje? Johan Cruyff, Frank Rijkaard, misimu miwili ya maajabu ya Pep Guardiola. Luis Enrique pia.

Walianzaje katika mechi zao tatu za awali katika hatua ya makundi ambayo utafafanuliwa chini. Je, walikaribia kufanya hiki alichokifanya Valverde? Twende sawa…

Cruyff (1992)

Mdachi huyo alianza kwa ushindi wa mechi mbili na kufungwa moja katika mechi tatu za ufunguzi wa michuano hiyo.

Alianza kwa kuichapa Hansa Rostock ya Ujerumani, mabao 3-0 kwenye mchezo uliopigwa Camp Nou kabla ya kukutana na kichapo cha bao 1-0 ugenini; mchezo wa tatu wa kundi hilo, Barcelona ikaitandika Kaiserslautern mabao 2-0 nyumbani, mchezo uliokuwa wa kwanza katika mzunguko wa pili hatua ya makundi.

Rijkaard (2006)

Katika msimu wa 2005/06 ambao Barca ilitwaa taji la michuano hiyo chini ya Rijkaard na ufundi wa miguu ya Ronaldinho, mchezo wa kwanza walianza kwa kuibamiza Werder Bremen mabao 2-0 kabla ya kuifunga Udinese mabao 4-1, lakini ikaja kutoa suluhu dhidi ya Panathinaikos katika mtanange wa tatu wa hatua ya makundi.

Guardiola (2009)

Mechi tatu za kwanza katika hatua ya makundi chini ya ‘mchawi wa benchi la ufundi’, Guardiola, zilianza kwa matokeo kama ya Cruyff. Guardiola aliwaongoza vijana wake kushinda mechi mbili za kwanza na kufungwa moja.

Kabla ya kuingia makundi, iliwabidi Barcelona wacheze na Wisla Krakow kwenye raundi ya tatu ya mchujo, ikishinda mchezo wa kwanza bao 4-0 na kupoteza 1-0 kwenye marudiano. Mechi yao ya kwanza ya makundi wakaitandika Sporting Lisbon bao 3-1.

Guardiola (2011)

Msimu wa pili wa mafanikio kwa Guardiola akiwa Barcelona, kikosi chake kilishinda mechi mbili za kwanza na sare moja.

Walianza kwa kuibanjua Panathinaikos mabao 5-1, kabla ya kutoshana nguvu na Rubin Kazan kwa bao 1-1. Mechi iliyofuata wakaifunga Copenhagen 2-0.

Enrique (2015)

Barcelona hii ya Enrique ilikuwa balaa na moto wa kuotea mbali, ambapo utatu wa washambuliaji uliojulikana kama ‘MSN’ ulimfanya kocha huyo apate mafanikio makubwa.

Enrique aliiwezesha Barcelona kutwaa mataji matatu kwa mara ya pili (baada ya Guardiola kufanya hivyo msimu wa 2008/09), lakini kikosi chake hakikuanza mechi zake tatu za awali kwenye makundi kwa kiwango cha moto sana, walishinda mechi mbili na kufungwa moja.

APOEL walikuwa wa kwanza kuvaana na Barca na wakapokea kichapo cha bao 1-0, lakini miamba hiyo ya Hispania ilijikuta ikionja joto ya jiwe kwa kufungwa bao 3-2 na PSG ugenini, kabla ya kujipoza na ushindi wa bao 3-1 dhidi ya Ajax, Camp Nou.

Valverde (2017)

Kwa sasa, Valverde, 53, ana rekodi safi baada ya kuanza kwa kuwachapa Juventus bao 3-0, wakasafiri hadi Ureno kuwafuata Lisbon ambapo waliibuka na ushindi wa bao 1-0 na mapema wiki hii wakawatandika Olympiacos bao 3-1.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.