Bongo Fc


Neymar anavyoishi kifalme ndani ya psg

PSG wamelipa Pauni 198 milioni na kuvunja rekodi ya uhamisho wa dunia kwa kumchukua Neymar kutoka Barcelona, katika dirisha kubwa lililopita la majira ya joto.

Hata hivyo, kwa sasa Neymar anaishi kistaa zaidi PSG na wanalazimika kuendana na masharti ambayo ameyaweka katika mkataba wake wa sasa na wababe hao wa Ufaransa. Mkataba huo unamfanya aishi klabuni hapo kistaa zaidi tofauti na wenzake.

Hakabi uwanjani

Kocha Mspanihola wa PSG, Unai Emery ana kazi ngumu pia ya kuishi ya Neymar. Analazimika kuiweka taaluma yake kando na kuishi na Neymar kwa kadri ambavyo mkataba unamwelekeza.

Kocha huyu kwa mujibu wa mkataba wa Neymar na PSG halazimiki kumpangia Neymar jukumu lolote lile la ulinzi. Neymar atakuwa akipokea mipira kutoka kwa wenzake akiwa huru na hana jukumu la kukaba pindi timu yake inapopoteza mpira.

Hachezewi rafu mazoezini

Kutokana na uchawi wake akiwa na mpira, Neymar amekuwa akichezewa rafu nyingi mazoezini na katika mechi. Wakati akikaribia kuondoka Barcelona alijikuta akikunjana na mlinzi mpya wa Barcelona, Nelson Semedo kutokana na rafu aliyomchezea mazoezini hapo.

Kwa mujibu wa mkataba wake wa sasa na PSG, Neymar hapaswi kuchezewa rafu yoyote mbaya au kukabwa ovyo akiwa mazoezini. Hii ina maana, benchi la ufundi linaweza kumpa adhabu kali mchezaji, ambaye atamchezea rafu Neymar.

Ana madaktari maalumu

Neymar amepewa madaktari wawili maalumu kwa ajili yake tu. Madaktari hawa hawajihusishi na wachezaji wengine na wanalipwa na PSG kwa ajili ya kazi ya kuhakikisha Neymar yupo fiti kabla na baada ya mechi.

Kabla ya Neymar inadaiwa mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Zlatan Ibrahimovic naye alishawahi kupewa upendeleo huo wa kuwa na madaktari wawili ambao, walikuwa wanamchunguza yeye tu huku wachezaji wengine wakichangia huduma za madaktari wengine waliopo klabuni hapo.

Begi la peke yake

Kutokana na kuwa na mikataba yake mingi binafsi inayompatia pesa ndefu, Neymar ameingia mkataba binafsi na PSG ambao, unampa ruhusa ya kuwa na begi lake binafsi lenye logo ya kampuni anazotangaza huku wachezaji wengine wakiwa wanabeba mabegi ambayo yana logo ya PSG.

Neymar pia anaruhusiwa kuwa na baadhi ya vitu ambavyo ni tofauti na wenzake pindi wanaposafiri kwa ajili ya mechi za ugenini.

Kupiga penalti zote msimu ujao

Hivi karibuni kulikuwa na mzozo mkubwa wa kugombea penalti kati ya Neymar na staa mwingine wa timu hiyo, Edinson Cavani. Ilikuwa ni katika pambano dhidi ya Lyon. Mwishowe Cavani alifanikiwa kupiga penalti hiyo.

Hata hivyo, huu ni msimu wa mwisho kwa mashabiki kushuhudia mzozo wa namna hiyo kwa sababu kuanzia msimu ujao, kwa mujibu wa mkataba Neymay ndiye atapiga penalti zote za PSG. Kwa msimu huu ameahidiwa kupiga asilimia 50 ya penalti zote na ndio maana ulitokea mzozo kama ule.

Msimu ujao Cavani na wachezaji wengine wote watalazimika kumwachia penalti zote Neymar, labda kama akiwa nje ya mechi.

Mastaa wenzake wakerwa

Habari za ndani kutoka PSG zinadai mastaa wengi wa klabu hiyo wamekerwa na jinsi ambavyo uongozi wa klabu hiyo umeamua kuwa na upendeleo maalumu kwa Neymar, tangu atue klabuni hapo. Mastaa wengi wanaamini soka ni mchezo wa timu na sio mchezaji mmoja mmoja na wamekiri Neymar amewagawanya kihisia ndani ya timu hiyo.

Katika mzozo wa upigaji penalti kati yake na Cavani, idadi kubwa ya wachezaji wa PSG walikuwa wamemuunga mkono Cavani katika mzozo huo na Neymar alilazimika kuomba radhi kwa Cavani baada ya kugundua alikuwa haungwi mkono na wachezaji walio wengi.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.