Bongo Fc


Zimbabwe, libya kushiriki chalenji

Timu za soka za Taifa za Zimbabwe na Libya zimethibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Chalenji, inayotarajiwa kuanza Novemba 25, mwaka huu, nchini Kenya, baada ya timu za Eritrea na Djibouti kujitoa.

Michuano hiyo, inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), inarejea ikiwa ni baada ya miaka miwili kupita tangu ilipofanyika mwaka 2015, nchini Ethiopia, katika Mji wa Addis Ababa.

Katika mashindano ya mwisho kufanyika, timu ya Taifa ya Uganda ndio waliibuka mabingwa kwa kuwafunga Rwanda bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali.

Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye, alithibitisha kuwa timu za Zimbabwe na Libya zitakuwa wageni waalikwa wa michuano hiyo, baada ya kuandika barua ya maombi.

“Kuna timu 12, lakini Libya na Zimbabwe watakuwa wageni waalikwa wa michuano hii. Walithibitisha kupitia barua zao walizotuandikia. Timu hizo zitachukua nafasi ya Eritrea na Djibouti ambazo zimeshindwa kuthibitisha ushiriki wao,” alisema Musonye.

Mbali na kuelezea timu zitakazoshiriki, Musonye pia alizungumzia kuhusu viwanja ambavyo vitatumika kwa michuano hiyo.

“Mapema leo (jana) tulitembelea Uwanja wa Bukhungu, ambao upo Kakamega na kufanya ukaguzi kwa sababu upo katika hatua za mwisho za matengenezo, tunaamini utakamilika mapema kabla ya michuano kuanza,” aliongeza katibu huyo.

Viwanja vingine ambavyo vitatumika ni Moi uliopo Kisumu, Afraha uliopo Nakuru na Mumias Sports Complex, ambao upo katika Mji wa Mumias.

Timu nyingine 10 zilizothibitisha kushiriki Chalenji ni wenyeji Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania, Zanzibar, Burundi, Ethiopia, Somalia, Sudan na Sudan Kusini, ambapo timu zote zitaanza kuwasili nchini Kenya Novemba 22, mwaka huu.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.