Bongo Fc


Yanga, mbeya city zaidi ya vita

Sare dhidi ya Singida United imeonekana kuwanyima raha Yanga na sasa timu hiyo imeweka mikakati ya kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Mbeya City.

Timu hizo zitaumana kwenye Uwanja wa Uhuru Novemba 19, mwaka huu katika mchezo wa raundi ya 10 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha Msaidizi wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya Michezoni ya SportPesa, Shadrack Nsajigwa, aliiambia BongoFC jana kuwa hawataki kuona wanapoteza pointi kwenye mchezo huo.

"Tunaendelea na mipango yetu, tunataka kuona tunapata pointi zote tatu kwenye mchezo huo ili kuendelea kubaki kwenye mbio za ubingwa," alisema Nsajigwa.

Alisema ana uhakika mchezo huo hautakuwa rahisi kwa kuwa Ligi Kuu msimu huu ni ngumu.

Nsajigwa alisema wameandaa programu ya mazoezi ambayo wanaendelea kuitekeleza huku wakimsubiri Kocha Mkuu, George Lwandamina aliyekwenda Zambia kwa matatizo ya kifamilia.

Naye Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, aliongeza kuwa Lwandamina anatarajia kurejea nchini leo kuendelea na majukumu yake.

Alisema kuwa taarifa za kuwa kocha huyo atakuja na mchezaji mmoja wa kimataifa kwa ajili ya kumsajili kwenye dirisha dogo la usajili linaloanza keshokutwa si kweli.

"Kocha anarudi kesho (leo) ila hakuna mchezaji anayekuja naye kama ambavyo imekuwa ikielezwa," alisema Hafidh.

Aidha, Hafidh alisema timu hiyo leo inaendelea na mazoezi baada ya jana kupumzika.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.