Bongo Fc


Lwandamina kutua leo kuiandaa yanga dhidi ya mbeya city, jumapili

Kocha wa Yanga, Mzambia George Lwandamina anatarajiwa kurejea leo Dar es Salaam kutoka kwao, Zambia ambako alikwenda kwa mazishi ya mpwa wake.

Lakini Lwandamina, mchezaji wa zamani wa Mutondo Stars, Mufulira Blackpool na Mufulira Wanderers pamoja na timu ya taifa ya Zambia, hataweza kuwahi mazoezi ya leo, bali atakuwa tayari kuanza kazi kesho.

Katika kipindi cha chote cha wiki nzima ya Lwandamina kuwa Zambia, kikosi cha Yanga kimekuwa kikiendelea na mazoezi chini ya makocha Wasaidizi, Mzambia mwingine, Noel Mwandila na wazawa, Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali.

Lakini katika mazoezi hayo, Yanga iliwakosa wachezaji wake wengi waliokuwa na timu za taifa ya U-23 na ya wakubwa, Taifa Stars.

Ikabidi wachezaji wa timu ya vijana, Yanga B wapelekwe kufanya mazoezi na wachezaji wachache wa timu ya wakubwa.

Yanga inatarajiwa kushuka dimbani Jumapili kumenyana na Mbeya City, Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam katika mfululizo wa Ligi Kuu.

Kwa ujumla baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kirafiki za kimataifa zikiwemo za kufuzu Kombe la Dunia, Ligi Kuu inatarajiwa kurejea wikiendi hii na Ijumaa Singida United wataikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Namfua, wakati Azam FC watakuwa wageni wa Njombe Mji FC Jumamosi Uwanja wa Saba Saba.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.