Bongo Fc


Arsenal v spurs… kwa sababu hizi, labda wenger afute matokeo

Na: Omary Ramsey
Email: omaryramsey@gmail.com

Baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa, sasa uhondo wa mikikimikiki ya Ligi Kuu England inarejea wikiendi hii na moja kati ya mechi kali ni ile ya ‘London derby’ kati ya Arsenal na Tottenham.

Mchezo huo utachezwa kesho na ni Arsenal ndio watakaokuwa wenyeji wa mahasimu wao hao wa jijini London.

Awali, Arsenal walionekana kuwatawala wenzao katika michezo mingi, lakini katika miaka ya hivi karibuni, ni kama Tottenham wamepindua matokeo.

Arsenal wataingia kwenye mchezo wa kesho wakiwa wanashika nafasi ya sita kwenye msimamo baada ya kujikusanyia pointi 29 katika michezo 11, ikiwa imefunga mabao 20 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 16.

Tottenham wanaoshika nafasi ya tatu, wana pointi 23 katika idadi hiyo ya michezo, nyavu zao zikifumaniwa mara saba na wao wakifunga mabao 20.

Hivyo, ni wazi safu za ushambuliaji za timu zote ziko sawa, ingawa Arsenal wameonekana kuwa na safu mbovu ya ulinzi kuliko wenzao hao.

Habari mbaya kwa mashabiki wa Arsenal ni kwamba huenda straika wao, Olivier Giroud, akashindwa kucheza baada ya kuumia akiwa na kikosi cha Ufaransa.

Kuna uwezekano pia wa kuendelea kumkosa Rob Holding, ingawa kuna taarifa kuwa David Ospina na Shkodran Mustafi watarejea kuivaa Spurs.

Kwa upande wa Tottenham, wao wana rundo la majeruhi kwani mbali na kuwakosa makipa, Hugo Lloris na Michel Vorm, haitakuwa na huduma ya Toby Alderweireld na Jan Vertonghen, huku kukiwa hakuna dalili ya kurejea kwa Victor Wanyama.

Hata hivyo, kuelekea mtanange wa kesho ambao utakuwa wa 12 kwa kila timu, mambo yameonekana kuwa mazuri kwa Spurs ya kocha Mauricio Pochettino.

Je, ni mambo gani hayo yanayoiweka Arsenal kwenye hatari ya kupoteza pointi tatu licha ya kwamba mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Emirates, mbele ya mashabiki wapatao 60,000?

Arsenal ‘nyanya’ kwa vigogoMsimu uliopita, Gunners waliambulia pointi tisa pekee kati ya 30 za michezo ya timu kubwa.

Vijana hao wa kocha Arsene Wenger, walishinda mechi mbili pekee kati ya 10 za ugenini dhidi ya ‘top six’, wakitoa sare tatu na kufungwa tano.

Rekodi ya Spurs ugeniniTangu kuanza kwa mwaka huu, Spurs ndio timu pekee ambayo imevuna pointi nyingi ikiwa ugenini. Kikosi hicho kimeshinda mechi 10 zikiwamo dhidi ya Chelsea na Manchester City.

Lakini pia, Tottenham ndiyo timu yenye mabao mengi katika mechi za ugenini, ikiwa imezifumania nyavu mara 37.

Kane kwenye ubora wakeLicha ya kuondoshwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya England kilichocheza na Ujerumani na Brazil, straika Harry Kane atakuwa uwanjani kesho kuwavaa Arsenal.

Msimu huu pekee Kane ameshafunga mabao 13 katika mechi 14, huku Alexandre Lacazette, Mesut Ozil na Alexis Sanchez wakiwa na jumla ya mabao tisa.

Mbali na hilo, kwa pamoja watatu hao wamemzidi Kane kwa asisti moja pekee. Kesho, atakuwa na msaada wa Christian Eriksen, Heung Min-Son na Dele Alli. Itakuwaje kwa Gunners?

Wenger kwa Pochettino hapinduiKatika michezo ya hivi karibuni, Pochettino amekuwa na rekodi nzuri kila anapokutana. Tangu alipotua Tottenham mwaka 2014, kocha huyo raia wa Argentina hajapoteza hata mchezo mmoja kati ya sita aliyovaana na Mfaransa huyo.

Kwa kipindi chote cha miaka mitatu, amekutana na mzee Wenger mara sita, akashinda mara mbili na kutoa sare nne. Katika sare hizo, tatu amezipata kwenye Uwanja wa Emirates, ikiwa na maana kwamba Pochettino hajawahi kufungwa kwenye dimba hilo.

Zaidi ya hapo, Wenger hajachekelea ushindi mbele ya Tottenham katika michezo ya Ligi Kuu kwa miaka mitatu sasa.


Facebook Twitter

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.