Bongo Fc


Bao la bocco linaondoa ‘stress’

Kwa mujibu wa vigezo vya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), bao la mshambuliaji wa Simba, John Bocco, ambalo alilifunga dhidi ya Tanzania Prisons wikiendi iliyopita na kuipa timu yake pointi tatu muhimu ugenini, huenda likaingizwa kwenye orodha ya mabao mengine makali yanayowania Tuzo ya Bao la Mwaka ya Puskas (FIFA Puskas Award).

Bao hilo pia limeelezwa na mashabiki wa soka, kuwa linaondoa ‘Stress’ (Yaani msongo wa mawazo), unaosababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo ukosefu wa pesa hasa wakati huu ambao watu wengi wanasema vyuma vimekaza (hali ni ngumu) kutokana na ugumu wa maisha.

Bocco alifunga bao hilo katika mazingira magumu yaliyomlazimu kutumia juhudi zake binafsi na kupachika mpira wavuni, zikiwa zimesalia dakika sita mpira umalizike.

Mchezo huo ulikuwa ni wa presha sana, Prisons walijitahidi kulinda lango lao huku wakisukuma mashambulizi upande wa Simba, hali iliyokuwa ikiwashtua vijana hao wa kocha, Joseph Omog na kuongeza umakini kadiri dakika zilivyosonga, kwani ilijulikana wazi kwamba wangeteleza tu nafasi yao ya kwanza wangeiweka rehani.Bao hilo la Bocco lilitokana na mpira mrefu uliotoka upande wa Simba kuelekea langoni mwa Prisons, ambapo dakika ya 84, Bocco na Laudit Mavugo walizua kizaazaa kwa Wajelajela hao ambao walizidiwa na presha ya mchezo.

Katika hali ya kushangaza zaidi, Bocco alitumia sekunde moja tu kugeuka akiwa kwenye pembe ngumu ndani ya boksi, huku mabeki wa Prisons wakiwa wamezuia takribani upande mzima ambao angeweza kuutumia kufunga kwa urahisi, lakini hakutaka kupoteza muda na kupiga shuti lililojaa wavuni.

Katika orodha ya mwisho ya mabao yaliyowania tuzo ya Puskas mwaka huu, bao la mlinda mlango wa Baroka ya Afrika Kusini, Oscarine Masuluke, nalo lilikuwemo, hivyo kuibua uwezekano wa kuona bao la Bocco likiingizwa mwakani, ambapo itakuwa ni mara ya nane kwa mchezaji kutoka Afrika kuiwania tuzo hiyo ya heshima.

VIGEZO AMBAVYO VINATAZAMWA NA FIFA KATIKA KUCHAGUA MABAO HAYO YA KUSISIMUA NI KAMA IFUATAVYO:

Liwe ni bao zuri (ufungaji wake uwe aidha shuti la mbali, ushirikiano wa timu nzima, tik taka, juhudi binafsi na kwa njia nyingine).

Lichaguliwe ‘bila kutofautisha ligi, jinsia au utaifa’.

Bao hilo lisiwe la kubahatisha, makosa ya mabeki, kuguswa na mchezaji mwingine au mchezaji kuotea.

Lazima lizingatie usawa wa michezo, kwa mfano mchezaji kuwa na tabia zisizofaa uwanjani au kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli.

Kwa mujibu wa Fifa, tayari bao hilo la Bocco linaonekana kufuzu vigezo muhimu na huenda likapendekezwa kuingia kwenye orodha ya mabao 10 bora ya awali ambayo husimamiwa na wajuzi hasa wa soka kama tuzo ya mwaka huu iliyoendeshwa na mkongwe wa zamani wa Newcastle United, Alan Shearer, nyota wa timu ya Taifa ya wanawake ya Marekani, Abby Wambach na straika wa zamani wa Man United, Henrik Larsson.


Facebook Twitter

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.