Bongo Fc


Mwakyembe awapa kazi kichuya, ajib

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amewapa kazi washambuliaji, Shiza Kichuya na Ibrahim Ajib, kuhakikisha wanaendeleza makali katika michuano ya Chalenji ili kuipa ubingwa Kilimanjaro Stars.

Washambuliaji hao ni miongoni mwa wachezaji 23 wanaounda kikosi cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, iliyoondoka jana jijini Dar es Salaam na Ndege ya Shirika la Kenya.

Kilimanjaro Stars itafungua dimba Jumapili kwa kucheza na timu ya Taifa ya Libya, ambao wanashiriki michuano hiyo kama mgeni mwalikwa.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha usiku na kuaga timu hiyo iliyofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Seascape, Mbezi Beach, Dar es Salaam, Mwakyembe alisema ana matumaini makubwa ya Kilimanjaro Stars kurejea na ubingwa kutokana na ubora wa wachezaji wanaounda kikosi hicho.

Mwakyembe alisema anafahamu kati ya timu zinazoshiriki michuano hiyo, inayozungumzwa zaidi ni Tanzania, hivyo ni jukumu la wachezaji kujituma na kuibuka na ushindi kila mechi watakayocheza.

“Nina matumaini makubwa na kikosi hiki, nimeangalia idara zote zimekamilika hasa safu ya ushambuliaji nimemwona Kichuya hapa na Ajib, naamini hamtawaangusha Watanzania, pigeni kila mtakayekutana naye,” alisema Mwakyembe.

Alisisitiza kuwa jambo la msingi ni kuzingatia nidhamu na kutodharau timu yoyote, kwani kila mechi ichukuliwe kama fainali au wanacheza na Brazil.


Facebook Twitter

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.