Bongo Fc


Sportpesa yakabidhi rasmi uwanja wa taifa

Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa jana ilikabidhi rasmi Uwanja wa Taifa kwa serikali baada ya kukamilisha marekebisho eneo la kuchezea yaliyofanyika kwa kipindi cha miezi mitatu.

Uwanja huo ambao ulianza kutumika mwaka 2007, umefanyiwa marekebisho makubwa na kampuni hiyo sehemu ya kuchezea na vyumba vya kubadilishia nguo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika kwenye uwanja huo, Temeke Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Utawala na Uendeshaji wa SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas, alisema kampuni hiyo imetumia pesa nyingi katika kuwekeza kwenye soka hapa nchini.

Alisema matengenezo yaliyofanyika kwenye uwanja huo nimakubwa na yameufanya uwanja huo kuwa wa kimataifa zaidi.

“Wakati tunajiandaa kuileta klabu ya Everton hapa nchini, wawakilishi wao walipokuja waliona uwanja wetu hauna vigezo, hivyo walitutaka kufanyia merekebisho kwa namna wanavyotaka wao ili timu hiyo iweze kuja. SportPesa tulifanya, hivyo na hata walipokuja mara ya pili waliukubali na timu ya Everton ikaja,” alisema Tarimba.

Alisema mara baada ya timu hiyo kuondoka, kwa kushirikiana na serikali waliufunga uwanja kwa ajili ya matengenezo makubwa ambapo sehemu ya kuchezea ilikwanguliwa yote na kuweka udongo na nyasi mpya.

“SportPesa imetumia zaidi ya shilingi bilioni nne kuwekeza kwenye soka hapa nchini, ikiwa ni pamoja na ukarabati wa uwanja huu, udhamini kwa klabu tatu za Yanga, Simba na Singida United, hakuna kampuni nyingine iliyoweza kufanya hivi na sisi kama SportPesa tunajivunia,” alisema Tarimba.

Akipokea uwanja huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema serikali imeridhishwa na juhudi za SportPesa katika kuendeleza soka hapa nchini.

“Kitu kizuri ni kwamba pamoja na kuwa uwanja huu umekarabatiwa, lakini pia tunao vijana sita ambao wamepatiwa mafunzo ya kuukarabati pale inapotakiwa na kwa sasa hatutakuwa na haja ya kuita watu kutoka nje, hii yote ni kazi ya SportPesa, kama serikali tunawashukuru sana,” alisema Mwakyembe.


Facebook Twitter

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.