Bongo Fc


Omog aikamua sh mil. 40 simba

Klabu ya Simba imelazimika kumlipa aliyekuwa Kocha Mkuu wao, Joseph Omog, kitita cha takribani Sh milioni 40 kutokana na kuvunja mkataba baina ya pande hizo mbili.

Uongozi wa Simba ulifikia uamuzi wa kuvunja mkataba wao na Omog mapema wiki hii kutokana na madai ya kutoridhishwa na mchango wake kikosini, ikiwa ni saa chache baada ya timu yao kuvuliwa ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam walipochapwa na timu ya Daraja la Pili ya Green Warriors ya Mwenge, Dar es Salaam kwa mikwaju ya penalti 4-3.

Taarifa za uhakika zilizolifikia BongoFC jana kutoka kwa kigogo mmoja wa Simba, zinasema kuwa Omog kwa mwezi alikuwa akilipwa Dola za Marekani 5,000, sawa na shilingi 11,165,700.

Alisema kwamba mkataba baina ya pande hizo mbili unaelekeza kuwa atakayevunja mkataba, atalazimika kumlipa mwenzake mshahara wa miezi mitatu.

Alisema uongozi wa Simba na Omog walikutana Jumamosi ya wiki iliyopita kwa ajili ya makubaliano ya kuvunja mkataba na kufikia uamuzi huo.

“Baada ya kukaa na kukubaliana pande hizo mbili, Simba inahitaji kumlipa fedha hizo ikiwa ni mshahara wa miezi mitatu kama ilivyo kwa makocha wengine wakivunjiwa mikataba yao,” alisema mtoa habari huyo.

BongoFC jana lilimtafuta kocha huyo ambapo alisema kuwa bado yupo nchini akiusubiri uongozi wa Simba umpe chake asepe.

Alisema kuondolewa kwake Simba amekupokea kwa mikono miwili akiamini ni maisha ya kawaida kwa makocha ambao wanaajiriwa kwa ajili ya kufukuzwa.

“Haya ni maisha, sijajua naondoka lini, bado nipo nchini hadi hapo uongozi (wa Simba) utakapokutana na kunipa haki zangu zinazostahili, sitaweza kusema ni kiasi gani,” alisema Omog.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.