Bongo Fc


Kuna de bruyne wa guardiola, halafu kuna salah wa watu wote...

Na: Omary Ramsey

Naheshimu kipaji cha Kevin de Bruyne. Ni mchezaji wa kipekee sana. Ni kocha gani duniani asiyependa kuwa na mchezaji wa aina yake?

Kasi, nguvu na uwezo wa kutumia miguu yote miwili kwa ufasaha, ni mambo yanayomfanya kuwa kiumbe hatari uwanjani.

Yuko katika kiwango bora sana msimu huu, lakini ukiniuliza leo hii ni mchezaji gani hatari zaidi kwenye Premier League, msimu huu, bila shaka nitakutajia jina la Mohammed Salah.

Wenye lugha za kukera kwenye soka, wanapenda kumuita ‘Egyptian Messi’. Ndio. Salah ndiye ‘Messi wa Misri’. Messi wa Afrika.

Kwanini Salah? Rudi tena na umtazame De Bruyne. Ni mchezaji anayeubeba mfumo wa Pep Guardiola.

Ndiye ‘creative hub’ ya Manchester City. Mipango yote ya Pep inatengenezwa kwenye kichwa chake.Yeye ndiye anayeamua mfumo wa City uwanjani. Bruyne ndiye mwenye jukumu la kuamua ni muda gani timu ikimbie, muda gani washambulie na kuzuia. Ni tofauti na Salah.

Jurgen Klopp hana mfumo unaoeleweka msimu huu. Anabadilika kutokana na mpinzani anayekutana naye.

Tangu mwanzo hakuwa amemwandaa Salah kuwa mdungaji wake. Akili yake iliwaza jinsi ya kurahisisha majukumu la Sadio Mane.

Lakini uwezo wa Salah umebadili kila kitu. Amekuja kuubadili mfumo na mipango ya Liverpool. Ameweka kila kitu kwenye rada yake. Mabao anayofunga ni matokeo ya ubora wake na si mfumo wa Klopp.

Ni rahisi Man City kucheza bila De Bruyne, lakini ni ngumu mno kwa Liver kung’ara bila Salah. Kwanini?

Bernado Silva anaweza kuifanya kazi ya De Bruyne. Ilkay Gundogan pia. Japo si kwa asilimia kubwa, lakini mfumo wa Pep hauwezi kuathirika sana kwa kumkosa Kelin.

Lakini nani mwenye uwezo wa kuvaa viatu vya Salah? Si ndani ya Liverpool tu, hata katika timu nyingine, yuko wapi mchezaji wa aina yake kwa sasa?

Labda Kylian Mbappe. Labda, lakini uwezo wa Salah wa kukimbia, kujitengenezea na kumalizia shambulizi lake, ni wa kipekee sana.

Wakati huu tukibakiza siku chache kusherehekea mwaka mpya, Salah ameshafunga mabao 20. Mara ya mwisho mchezaji wa Liverpool, kufanya hivyo ni msimu wa 1986-87. Miaka 30 iliyopita.Liverpool wana bahati kuwa na Salah msimu huu. Afrika tuna bahati pia kuiona Misri inayokwenda Urusi, ikiwa na Salah kwenye kikosi chake. Kwanini nisiwape nafasi ya kufanya vyema?

Misri ya leo ni tofauti na ile ya jana na juzi. Tofauti ndogo sana. Leo tuna Misri ya Mohamed Salah na nyakati zile tulikuwa na Misri na kina Mohamed Aboutrika.

Leo tuna Misri ya Hector Cuper na nyakati zile tulikuwa na Misri ya Hassan Shehata.

Misri ya Aboutrika na Shehata ilikuwa ikicheza soka la Afrika katika tamaduni zake na miiko yake. Hii ya sasa ina mchanganyiko tamaduni tatu tofauti tofauti duniani.

Itazame Misri ya Cuper. Hawachezi tena kwa ajili ya kuwaburudisha mashabiki jukwaani, wako kwa ajili ya kupata matokeo. Asilimia 80 ya soka lao limetawaliwa na mbinu.

Wanacheza kwa kuvizia mno. Mara nyingi utawaona wakikaa nyuma na kuzuia. Wana ukuta imara kweli kweli. Ni katika mchezo mmoja tu kati ya 30 waliyocheza chini ya Hector Cuper, ndio wamefungwa zaidi ya bao moja.

Wengi wamekuwa wakimponda Cuper kwa mbinu hii ya kupaki basi, lakini hakuna anayejiuliza ni vipi katika kipindi kifupi baada ya kumaliza machafuko nchini kwao, Misri wamecheza fainali ya Afcon na kufuzu Kombe la Dunia. Hakuna anayetaka kujua hili.

Tangu Cuper aichukue Misri, asilimia 63 ya mechi zake ni ushindi tu. Hakuna anayetaka kujua na hili pia.

Misri wanakwenda Urusi wakiwa kamili. Pengine kamili kuliko kipindi chote kile cha ushiriki wao wa michuano mikubwa. Wanakwenda Urusi wakiwa na kikosi chenye mchanganyiko wa vijana na wakongwe.

Golini wanaye Essam El-Hadary ambaye bila shaka ataweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa kucheza Kombe la Dunia. Atakuwa na miaka 45.

Mbele yake watasimama wanaume wawili wagumu, Rami Rabia na Ahmed Hegazi, anayekipiga katika klabu ya West Brom.

Eneo la katikati litakuwa chini ya kiungo wa Arsenal, Mohamed Elneny na fundi mwingine anayekipiga katika klabu ya Al Ahly, Abdallah Said. Huyu ana miaka 32. Ana uzoefu wa kutosha pia.

Safu ya ushambuliaji, bila shaka Wamisri wote watakuwa wakiomba dua Mohamed Salah abaki katika kiwango chake cha sasa.

Ni fahari kiasi gani kuona raia wa Afrika akiwa mchezaji anayeogopwa zaidi kwenye Premier League? Hakuna beki pale England, mwenye hamu ya kukutana na Salah.

Pembezoni mwa uwanja, Cuper anaweza kuchagua wawili kati ya Ramadan Sobhi, Kahraba na Mahmoud Hassan “Trezeguet”. Kwanini tusiihofie Misri?

Katika mfumo wa 4-2-3-1, Misri ya Hector Cuper na Mo Salah, inakwenda kuitetemesha dunia. Naamini hili.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.