Bongo Fc


Uchambuzi: hili dirisha dogo litawaumiza sana watu

Asikudanganye mtu, utamu wa soka barani Ulaya huanza nyakati hizi. Uwanjani kinapigika, ofisini kinapiga pia. Nani kucheka nani kuumizwa kwenye usajili wa dirisha dogo?

Ni nafasi kwa klabu kununua, kuuza, kutoa kwa mkopo baadhi ya wachezaji, lengo likiwa ni kupata mafanikio mwishoni mwa msimu. BongoFC tumekuandalia chambuzi fupi ya ishu zote ambazo ungependa kuzijua katika dirisha hili la usajili.

Usajili unafunguliwa lini?

Haijalishi itakapokukutia saa 5: 59 usiku wa leo, unachotakiwa kufahamu ni kuwa, muda utakaoanza kusherehekea mwaka mpya wa 2018, ndio dakika hiyo hiyo, dirisha dogo la usajili barani Ulaya hufunguliwa.

Utafungwa lini?

Timu zitaruhusiwa kufanya sajili zao kwa njia za mtandao mpaka usiku wa Januari 31, saa sita usiku. Baada ya hapo dirisha litafungwa rasmi.

Je, Ligi za Ulaya zinapishana siku za kufungua na kufunga usajili?

Ligi kubwa tano barani Ulaya zote zitafungua na kufunga dirisha dogo la usajili sawa sawa. La Liga, Ligue 1, Serie A, Bundesliga na Premier League, usajili utafunguliwa Januari mosi na kufungwa Januari 31.

Ni Ureno pekee ambayo dirisha lao la usajili hufungwa Januari 2.

Tutegemee tena fujo za Wachina?

Kwenye misimu ya hivi karibuni tumeshuhudia jinsi Wachina walivyolitikisa dirisha dogo la usajili kwa kumwaga fedha za maana. Nyota wawili wa Chelsea, Oscar na Ramires, walitimka England na kujiunga na klabu za China baada ya kupewa fungu kubwa la mishahara.

Licha ya dirisha la usajili China kuwa wazi mpaka Februari 28, ni ngumu sana safari hii kuona wakifanya fujo sokoni na hii ni kutokana na sheria zilizowekwa na Shirikisho linalosimamia ligi ya nchini humo.

Unajua ishu ikoje? Kama klabu italipa dau la usajili chini ya pauni milioni 5.3 kwa ajili ya mchezaji basi watatakiwa kutoa kiwango hicho cha pesa kwa ajili ya kusaidia soka la vijana.

Na endapo klabu italipa zaidi ya pauni milioni 5.3 kwa usajili, italazimika pia kutoa kiwango kama hicho kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya soka la China. Hii ina maana ukilipa pauni milioni 50 ya usajili, unatoa pauni milioni 50 ya kukuza soka.

England watavunja rekodi ya usajili?

Katika dirisha kubwa la usajili, timu za Premier League zilitumia pauni bilioni 1.4 ni ngumu kuona rekodi hii ikivunja kwenye dirisha dogo la usajili, lakini kwa uwendawazimu wa soka hivi sasa, lolote linaweza kutokea.

Januari mwaka huu, timu za Premier zilifanya usajili wa pauni milioni 215 tu. Nyakati hizi tayari Liverpool peke yao wameshatumia pauni milioni 75 kumsajili beki wa Southampton, Virgil van Dijk.

Nyota wanaoweza kuhama?

Yako majina mengi mno, ndani na nje ya Premier League. Kiungo Mesut Ozil na Alexis Sanchez, ni miongoni mwa mastaa wakubwa wanaotajwa kutikisa dirisha hili.

Nyota wengine walio kwenye orodha hiyo ni Luke Shaw, Henrikh Mkhitaryan, Julian Draxler, Philippe Coutinho na Javier Pastore.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.