Bongo Fc


Makala: mo salah ‘messi wa anfield’

Wapinzani wana kazi mbili kubwa za kufanya siku hizi wanapokwenda Anfield. Kwanza ni kucheza dhidi ya Liverpool na pili ni namna ya kumzuia Mohammed Salah.

‘Ustadh Salah’ kama anavyoitwa katika vibandaumiza vingi nchini. Achana na mabao ya Harry Kane, achana pia na kasi ya Kevin de Bruyne, Mo Salah ndiye mchezaji hatari zaidi kwenye Premier League msimu huu. Namba zinazungumza!

Anawapa raha Liverpool. Anafunga na kutengeneza mabao kila siku. Haikushangaza sana mashabiki wa Majogoo hao wa Jiji la Liver, kumpachika jina la ‘Messi wa Anfield.’

Safari yake kutoka Misri hadi Ulaya ni kielelezo tosha cha ubora huu tunaoushuhudia leo hii. Salah alianza kuamini tangu utotoni.

Kabla ya kuwa Waziri Mkuu wa Misri, Ibrahim Mahlab, alikuwa Mwenyekiti wa klabu ya El Mokawloon. Timu ya utotoni ya Mohammed Salah.

Taarifa zinaonyesha kuwa 2011 klabu kubwa za Misri, Zamalek na Al-Ahly zilituma ofa ya maana kwa ajili ya kuihitaji saini yake lakini Mahlab alizipiga chini akisisitiza kiwango cha Salah ni cha kucheza Ulaya.

“Mahlab alikuwa na hisia kuwa Salah ameshafika kiwango cha kucheza Ulaya,” alisema Alaa Nabil aliyekuwa Mkurugenzi wa ufundi wa kikosi cha El Mokawloon na kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Misri. ‘Aliaminia angefanikiwa zaidi akiondoka Afrika.

‘Salah hakujua angeondoka vipi Misri wakati ule, lakini Mahlab aliendelea kumhakikishia kuwa iko njia ya kufanikisha hilo.

Liver waifukuzia saini yake kwa miaka minne

Hatimaye Salah alijiunga na FC Basel ya Uswisi na hapa ndio kwa mara ya kwanza mawakala wa Liverpool walipoanza kumfuatilia.

Katika mechi za Kombe la Uropa, Basel walipocheza dhidi ya Tottenham na Chelsea, wawakilishi wa Liverpool walisafiri kumfuatilia na mara kwa mara walikuwa wanakwenda pia mazoezini kumtazama.

Hapa Chelsea walipowapiga bao na kumsajili mwaka 2014, Liverpool hawakukata tamaa ya kuendelea kumfuatilia. Na alipojiunga na Fiorentina na Roma, skauti mkuu wa Liverpool, Barry Hunter na Mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo Michael Edwards, waliupasha uongozi kuwa wafanye kila linalowezekana kumnasa winga huyo.

“Kwa miaka minne, siku tano za kila wiki nilitoka nyumbani saa tatu asubuhi na kutembea kwa saa tano kufika mazoezini.

“Kawaida mazoezi huanza saa tisa na nusu au saa kumi, hivyo nilijitahidi kuwahi mapema. Ningemaliza mazoezi saa 12 jioni kisha kuanza tena safari ya kurejea nyumbani.

“Saa nne na nusu usiku ningefika nyumbani kisha nakula, nalala na kujiandaa na safari nyingine siku inayofuata. Yalikuwa maisha yangu ya kila siku na nilishazoea,” maneno ya Mohammed Salah, alipofanya mahojiano na mtandao rasmi wa klabu ya Liverpool.

Ni stori inayokupa taswira ya magumu aliyopitia, lakini inakufunza pia jitihada mara zote hulipa.

Salah alizoea kutoka nyumbani saa tatu asubuni na kurejea saa nne na nusu usiku kwa ajili ya kufanya mazoezi. Angebadilisha zaidi ya mabasi matano kila siku njiani.

“Nilianza kufanya mazoezi katika kiwanja cha karibu na nyumbani. Ni umbali wa nusu saa tu kutoka katika kijiji chetu cha Basyoun,” aliongeza Salah, mwenye mabao 17 na asisti tano kwa dakika 1596 alizocheza kwenye Premier League msimu huu.

“Baadaye nilipata timu katika mji wa Tanta, ni mwendo wa saa moja na nusu kutoka nyumbani. Sikukaa sana nikajiunga na timu Arab Contractors iliyokuwa Cairo. Hapo ndio nililazimika kutembea mwendo mrefu kutoka nyumbani kwa ajili ya kwenda kufanya mazoezi.

Apewa ruhusa na mkuu wa shule kukaa darasani masaa mawili tu

Nililazimika kuondoka shule mapema ili niwahi mazoezini. Nilikuwa na barua rasmi ya mkuu wa shule kwa ajili hiyo hivyo shule nilifika saa moja asubuhi na kutoka saa tatu.

Naikumbuka ile barua ya mkuu wa shule iliandikwa ‘Mo aruhusiwe kuondoka mapema ili awahi mazoezini.

Nilikaa shule kwa masaa mawili tu. Sijui maisha yangekuaje sasa kama ningefeli kwenye soka!

Sasa tunamzungumzia mchezaji bora wa Afrika, mchezaji bora wa mwezi Novemba, kwenye ligi kubwa ya England. Sasa tunamzungumzia Mo Salah, anayefunga anavyojisikia.

Hili halijatokea kwa bahati mbaya. Tangu utotoni Salah alikuwa na ndoto ya kuwa mchezaji bora duniani.

“Kama nilivyosema, ilikuwa ngumu nyakati zile lakini sikukata tamaa. Nilitamani kuwa mchezaji mkubwa siku moja, mchezaji wa kipekee kidogo,” alisema Salah.

“Nawaambia ukweli, nilikuwa nikitamani kuwa mkubwa siku moja lakini sikufikiria kama ningekuwa hapa leo hii. Kila kitu kilikuwa ndoto kwangu nilipokuwa na miaka 14, lakini niliishi na imani kuwa nitafanikiwa. Namshukuru Mungu kwa yote.”

Hii ndio safari ya Mo Salah.

Alianza soka akiwa beki tatu, ilikuwaje akawa straika?

“Nilipokuwa kocha wa kikosi cha vijana U -16 cha Arab Contractors, nilikuwa na mabeki watano wa kushoto na Salah alikuwa mmoja wao,” alieleza Said El-Shishini, kocha mkuu wa klabu hiyo.

Arab Contractors, kwa sasa inafahamika kama El Mokawloon FC, ndio klabu ya kwanza ya Salah kufundishwa vitu vya msingu kwenye mpira.

El-Shishini anaeleza jinsi mambo yalivyokuwa katika miaka miwili aliyokaa na shujaa huyu wa Misri.

“Mchezo mmoja tulicheza dhidi ya ENNPI, timu ya vijana imara sana wakati huo. Tulishinda mabao 4-0 na Salah alianza kikosi cha kwanza akiwa beki wa kushoto.

“Nakumbuka alipoteza nafasi tano za kufunga akiwa yeye na golikipa wa ENPPI.

“Kwangu kitu kikubwa haikuwa nafasi alizopoteza bali uwezo wake wa kukokota mpira kutoka nyuma mpaka kubaki na golikipa. Kilikuwa kitu cha kipekee sana kwa kila aliyehudhuria mechi ile.

“Lakini baada ya mchezo, nilimuona Salah akijiinamia na kulia kwa nafasi alizokosa. Nakumbuka nilitoa paundi 25 za Misri kwa straika aliyefunga mabao matatu na Salah nilimpa paundi 25.

El-Shishini anasema ule ndio ulikuwa mwanzo wa mabadiliko ya Salah, kwa kuanza kuchezeshwa katika nafasi za mbele.

“Kutoka siku ile nilifanya maamuzi ya kumpa Salah katika wingi ya kulia,” alisema El-Shishini. “Nilimwambia angekuwa mfungaji bora wa timu zote mbili, kikosi chetu cha U -16 na Ligi ya taifa ya vijana U-17. Nilikuwa kocha wa timu zote mbili na nilimpanga Salah mbele.

“Mwisho wa msimu alifunga jumla ya mabao 35 na tangu hapo ameendelea kufunga kila siku bila kuchoka.

Salah kwenye Premier League, 2017-18

Dakika alizocheza 1596

Mabao 17

Asisti 5

Mashuti 66

Mashuti yaliolenga lango 41


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.