Bongo Fc


Guardiola katika ufalme mpya ulaya

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, ndiye anayeonekana kuwa na mafanikio ya haraka na makubwa ndani ya muda mfupi ikilinganishwa na baadhi ya makocha wengine wakubwa barani Ulaya.

Uwezo wake ndio unaomfanya kuwa mtu wa tofauti, lakini pia mtawala kwenye soka la Ulaya akiwa na mafanikio makubwa kwenye Ligi Kuu tatu tofauti ambazo pia ni kubwa na zenye timu imara.

Ligi hizo ni Hispania akiwa kwenye kikosi cha FC Bacelona ambayo aliitengeneza na kuwa timu kubwa kwenye kila kitu, lakini iliyoweza kutwaa mataji makubwa tofauti ndani na nje ya Hispania.

Hili lilimfanya akawa mtu wa tofauti na akaendelea kuwa kocha mwenye kukubalika lakini mwenye mafanikio pia, ambapo timu kadhaa zilianza kuona uwezo wake na kuhitaji huduma yake.

Baada ya kukaa Barcelona na kutwaa mataji kadhaa ikiwamo La Liga mara tatu, Copa del Rey mara mbili, UEFA Champions League mataji mawili, UEFA Super Cup mara mbili na ubingwa wa Klabu Bingwa ya Dunia mataji mawili.

Alipohamia nchini Ujerumani mwaka 2013 katika kikosi cha Bayen Munich, alifanikiwa kuitawala Bundesliga. Katika muda aliokaa ndani ya Ujerumani akiweza kutwaa mataji matatu ya ligi kuu, taji la DFB-Pokal mara mbili, UEFA Super Cup taji moja na Klabu Bingwa ya Dunia taji moja.

Kimsingi kwa takwimu hizi ni wazi kwamba Guardiola aliweza kufanya atakavyo kwa timu za Ujerumani lakini pia hata timu za Ulaya, haya yamekuwa ni mafanikio makubwa kwake ambayo makocha wengi wameshindwa kuyafikia.

Kwa wakati huu sasa yupo kwenye kikosi cha Manchester City akiwa na rekodi ya tofauti ambayo ni ya pekee msimu huu, kwani hajafungwa hata mechi moja kati ya mechi 21 ambazo kikosi chake kimeshacheza.

Kwenye mechi hizo 21, Machester City imefanikiwa kukusanya jumla ya pointi 59 lakini ikishinda michezo 19 huku ikipata sare mechi mbili na kufanikiwa kufunga mabao 61, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12.

Hizi ni takwimu ambazo zinamfanya Guardiola kuwa mfalme kwenye soka la England, ikiwa ni msimu wake wa pili kwenye ligi hiyo ingawa msimu wa mwaka jana hakuweza kufanya vizuri na ilichangiwa na mambo mbalimbali ikiwemo ugeni katika ligi lakini alikuwa na kikosi ambacho hakuwa amekisajili.

Lakini inaonekana wazi kuwa msimu huu kuna kitu anataka kuiambia dunia kwamba, yeye ni mtu wa aina gani hasa kwenye suala la ubora na kuweza kufanya kile anachokitaka lakini kubwa likiwa ni kutwaa mataji.

Hilo ameliweza na ndiyo maana leo inaonekana Machester City ipo kwenye kiwango bora, ikipata matokeo bora bila kujali inacheza kwenye uwanja gani.

Hilo limekuwa ni jambo ambalo limemfanya Guardiola kuwa na ufalme wake ndani ya Ulaya lakini inaweza kuwa jambo la uhakika zaidi kama akifanikiwa kutwaa ubingwa wa England msimu huu, jambo ambalo linaonekana litakuwa hivyo tena mapema.

Kwa timu nyingine ambazo zinaonekana kupambania nafasi hiyo hazijaweza kuonyesha uwezo mkubwa zaidi ya kikosi cha Guardiola, kwani Chelsea inashika nafasi ya pili.

Tayari imeshacheza mechi 21 ambapo kati ya hizo imeshinda michezo 14 na kupata sare mechi tatu huku ikifungwa mechi nne ambazo imeifanya kufunga mabao 39, ikifungwa mabao 14 lakini ikiwa na pointi 45.

Manchester United nayo ikiwa nafasi ya tatu imeshacheza mechi 21 na kushinda 13, lakini imevuna sare tano huku mechi tatu ikifungwa ikiwa na mabao 43 ya kufunga na kufungwa mabao 16 na kujikusanyia pointi 44.

Kinachotakiwa kufanyika ili Manchester City isiweze kutwaa ubingwa msimu huu ni yenyewe ipoteze zaidi ya mechi nne mfululizo, lakini hizo nyingine nazo ipate ushindi bila ya kupata sare wala kufungwa.

Kinyume na hapo suala la Guardiola kuwa mfalme mpya ndani ya EPL ni jambo ambalo linaonekana halizuiliki kwa sasa kutokana na ubora wa kikosi chake ambacho kinaonekana kupata matokeo kulingana na aina ya mechi bila kujali ukubwa au udogo wa timu, huo ndiy ufalme wa Guardiola anautengeneza kimya kimya.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.