Bongo Fc


jesse lingard ndani ya 'gemu' hizi 5 zilizompa ustaa old trafford, epl

Nyota Jesse Lingard ameibuka kuwa staa mpya kwenye kikosi cha kocha Jose Mourinho.

Fowadi huyo ameshapachika mabao saba katika mechi tisa zilizopita, yakiwamo matano ya ugenini.

Siri kubwa ya mafanikio ya Lingard ni Mourinho ambaye amembadilishia nafasi uwanjani. Msimu uliopita, nyota huyo mwenye umri wa miaka 25, alikuwa winga lakini mwezi uliopita alianza majukumu ya kucheza kama straika.

Lingard ambaye ana historia ya kutolewa kwa mkopo mara nne, ndiyo kwanza amecheza mechi 69 za Ligi Kuu England, akimpita nne Marcus Rashford ambaye ni mdogo kwake kwa miaka mitano.

Kwa upande mwingine, makala haya yamechungulia mechi zilizompa jina kubwa Lingard na kumfanya sasa awe staa kwenye kikosi cha Mashetani Wekundu wa Old Trafford.

Swansea 0-2 Man United

Huo ulikuwa ni mchezo wa raundi ya nne ya Kombe la Ligi na ilikuwa ni baada ya Lingard kutoingia ‘first eleven’ kwa takribani mwezi mmoja.

Sababu ya kutomtumia kwa kipindi chote hicho ilikuwa kiwango kibovu alichokionesha katika mchezo wa Super Cup dhidi ya Real Madrid.

Dhidi ya Swansea katika Uwanja wa Liberty, Mourinho akampa nafasi ya kuanza nyuma ya Marcus Rashford na Anthony Martial.

Lingard aling’ara vilivyo na kumkosha Mourinho kwani ndiye aliyepasia nyavu mara mbili katika ushindi wa mabao 2-0.

Watford 2-4 Man United

Ilikuwa Novemba 28 mwaka jana na ulikuwa ni mchezo wa pili wa Ligi Kuu kwa Lingard kuingia kikosi cha kwanza tangu kuanza kwa msimu huu wa 2017-18.

Watford walishachapwa mabao 3-0 lakini waliweza kupambana na kuchomoa mawili. Hata hivyo, zikiwa zimebaki dakika tano kabla ya mwamuzi kuumaliza mchezo, Lingard alifunga na kuipa Man United ushindi wa mabao 4-2.

Kilichowafurahisha mashabiki wa Old Trafford ni staili ya bao hilo, kwani alichomoka na mpira kutoka katikati ya uwanja na kumtungua kirahisi kipa wa Watford, Heurelho Gomes.

Arsenal 1-3 Man United

Siku nne baada ya kuimaliza Watford, Lingard akaingia Emirates kuivaa Arsenal, mchezo ambao pia alifanya vizuri na kuzidi kuwateka mashabiki wa Man United.

Katika mchezo huo, Mourinho alimchezesha namba 10, nyuma ya straika wa bei mbaya klabuni hapo, Romelu Lukaku.

Lingard alifunga mabao mawili huku jingine la Man United likifungwa na Antonio Valencia, Arsenal wakipata la kwao kupitia kwa Mfaransa Alexander Lacazette.

Huo ulikuwa ni ushindi wa kwanza kwa Mourinho katika mechi za ugenini dhidi ya timu vigogo.

Man United 1-2 Man City

Ni mchezo uliomaliza rekodi ya Man United kucheza mechi nyingi bila kufungwa. Lingard hakuwa kwenye kiwango kizuri lakini mchango wake ulionekana wazi kikosini.

Lingard aliweza kuwafanya Marcus Rashford, Anthony Martial, Juan Mata na Henrikh Mkhitaryan, waonekane uwanjani.

Ni kweli Man United walipoteza mtanange huo, lakini Lingard alifanya kazi iliyompa heshima kubwa mbele ya Mourinho na mashabiki wa timu yake hiyo.

Everton 0-2 Man United

Wakati Everton wakihaha kuchomoa bao la Anthony Martial, Lingard aliwakatisha tamaa katika dakika ya 81 baada ya kuihakikishia Man United ushindi wa mabao 2-0.

Lakini pia, akapachika tena katika mchezo dhidi ya West Brom ambapo Man United waliokuwa ugenini walishinda mabao 2-1.

Ukiacha huo, mchezo dhidi ya Burnley ulimshuhudia nyota huyo akitokea benchi na kupasia nyavu mara mbili na kuiwezesha Man United kuambulia sare ya mabao 2-2.

Kabla ya kuingia kwake uwanjani katika mtanange huo uliochezwa ‘Boxing Day’ katika Uwanja wa Old Trafford, tayari Man United walishatandikwa mabao 2-0.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.