Bongo Fc


Hanspope: simba kuna tatizo

Siku moja baada ya kuondolewa kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, amesema kuwa inawezekana kuna tatizo ndani ya kikosi cha timu hiyo.

Simba inayodhaminiwa na kampuni ya Sportpesa juzi, ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa URA na hivyo kutupwa nje ya michuano hiyo.

Akizungumza na kituo kimoja cha redio cha jijini Dar es Salaam, Hanspope, alisema kwa namna hali ilivyo kwa baadhi ya wachezaji inaashiria kuna tatizo hasa baada ya baadhi ya wachezaji waliocheza kwenye mchezo wa juzi, walipofanyiwa mabadiliko hawakutaka kukaa kwenye benchi la timu hiyo, kama ilivyo kawaida na kwenda kukaa jukwaani.

“Haiwezekani mchezaji anatolewa, badala ya kukaa na wenzake kwenye benchi anaenda kubadilisha nguo na kukaa jukwaani huku mchezo ukiendelea, hiyo inaonyesha kuna kitu, tutafuatilia kuona tatizo ni nini,” alisema Hanspope.

Nahodha wa zamani wa timu hiyo Jonas Mkude na mshambuliaji Shiza Kichuya, baada ya kufanyiwa mabadiliko kwenye mchezo huo hawakukaa kwenye benchi na walionekana kwenye jukwaani.

Hanspope alisema kuwa wameumizwa kutolewa hatua ya makundi kwenye michuano hiyo, lakini hakuna namna na wanapaswa kuangalia mbele kwenye ligi kuu Tanzania Bara.

Simba ambayo inaongoza kwenye msimamo wa ligi ilirejea Dar es Salaam jana tayari kwa maandalizi ya michezo yake ya ligi kuu.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.