Bongo Fc


Kocha simba aishi kifahari d’salaam

Simba inajiweza kifedha kwa sasa asikwambie mtu. Katika kuthibitisha hilo imempa maisha ya kifahari kocha wake, Masudi Djuma, japo taarifa za chini chini zinadai kocha huyo wala hayafurahii hata kidogo.

Timu hiyo ya pili kwa kutwaa mataji mengi ya Ligi Kuu Bara imemkodia kocha huyo chumba katika moja ya hoteli za kisasa jijini Dar es Salaam (jina tunalo) ambapo gharama ya kulala usiku mmoja inakaribiana na mshahara wa waajiriwa wengi tu mjini.

Pamoja na kwamba kocha huyo amekuwa akiwasisitiza mabosi wake kuwa hafurahii maisha ya hotelini na kushinikiza wamtafutie nyumba, bado ameendelea kuishi hotelini hapo kwa siku 86 sasa.

Kwa mujibu wa taarifa ambayo imetolewa na Gazeti la Mwanaspoti ni kwamba awali mabosi wa Simba walimtafutia kocha huyo nyumba, lakini walichelewa kwenda kuilipia hivyo ikawahiwa na mteja mwingine. Imeelezwa.

Hata hivyo zipo taarifa pia kwamba kitendo cha Simba kuvurunda kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi nacho kimechelewesha mchakato wa kocha huyo kutafutiwa nyumba pamoja na gari ya kutembelea hivyo kuendelea kuishi hotelini hapo.

Kocha huyo ambaye alitua nchini Oktoba 19 mwaka jana kuchukua nafasi ya Mganda Jackson Mayanja, amekuwa akiishi hotelini hapo katika chumba ambacho kina kila kitu ndani ikiwemo sehemu ya kufanyia kazi na vikao vifupi.

Kwa mujibu wa mmoja wa wahudumu wa hoteli hiyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake aliliambia Gazeti hilo kuwa kocha huyo bado yupo hotelini hapo tangu alipotua nchini na sasa ni siku ya 86 (hadi jana Alhamisi).

Mhudumu huyo alisema kuwa kwa siku Simba hulazimika kulipia Sh179,000 ingawa alidai kwa mtu ambaye ni mteja wao wa siku nyingi kunakuwepo na punguzo za asilimia kadhaa.

Kwa hesabu za haraka, tangu kocha huyo Mrundi aanze kukaa hotelini hapo, Simba itakuwa imelipia kiasi cha Sh15.3 milioni (kabla ya punguzo), achilia mbali gharama nyingine.

“Ni kweli kocha wa Simba bado yupo hapa, ni mteja wetu mzuri maana tunaingiza pesa, nafikiri kuna punguzo ambalo wamepata ila sijajua ni kwa asilimia ngapi maana mimi sio Mtendaji Mkuu wa hoteli hii japo baadhi ya mambo nayafahamu,” alisema mhudumu huyo.

Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alisema kwa sasa hawezi kuzungumza chochote ila atatoa taarifa rasmi baada ya siku tatu juu ya maisha halisi ya kocha huyo.

Kwa upande wake Djuma, alikiri kuishi hotelini.

Mwanaspoti linafahamu kocha huyo bado hajapewa hata gari ya kutembelea kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Joseph Omog. Taarifa ambazo tunazo ni kwamba Djuma anahitaji gari la kifahari jambo ambalo linachelewesha mchakato wake.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.