Bongo Fc


Real yachapwa, zidane njia panda

Na: Omary Ramsey

Wakati mwingine maisha huwa yanaamua tu kuwa magumu. Ni kama ambavyo yamemgeuka kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane.

Maisha ya Zidane ndani ya klabu hiyo sasa yamekuwa magumu kama mfupa wa kuku wa kienyeji. Timu yake inashika nafasi ya nne katika La Liga tena ikiwa imeachwa pointi 16 na vinara Barcelona.

Pamoja na kwamba Madrid ina mechi moja mkononi, lakini kipigo cha bao 1-0 walichokipata jana kutoka kwa Villarreal kinazidi kuwaweka njia panda mabingwa hao wa La Liga na Ligi ya Mabingwa.

Bao la Pablo Fornals katika dakika 87, lilitosha kuwapa Villarreal ushindi muhimu dhidi ya Real kwenye Uwanja wa Bernabeu.

Madrid haichezi soka safi na la kuvutia tena. Washambuliaji wa Madrid wamekuwa butu msimu huu na mpaka sasa wakiwa wamecheza mechi 17 za La Liga si Cristiano Ronaldo wala mshambuliaji mwingine wa timu hiyo aliyeweza kufunga mabao zaidi ya saba.

Katikati ya wiki hii inayomalizika Madrid ilitoka sare ya mabao 2-2 na Numancia inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo.

Pamoja na kwamba Madrid ilitinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Mfalme, kitendo cha kutoka sare nyumbani na timu hiyo kimewafedhehesha sana mashabiki wake.

Maisha yanaonekana kumgomea Zidane sasa. Licha ya kwamba alishinda mataji mawili ya UEFA, mawili ya Klabu Bingwa Dunia na moja la La Liga katika kipindi cha miaka miwili aliyokaa klabuni hapo, mambo si mazuri.

Bila usajili wa maana kwenye dirisha hili, maisha ya Zidane yatakuwa mafupi sana klabuni hapo.

Kumbuka kwamba kwenye hatua ya 16 ya UEFA, Madrid imepangwa na PSG yenye Neymar, Kylian Mbappe na Edson Cavani.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.