Bongo Fc


Ukweli mfaransa wa simba huu hapa..

Wakati kocha mpya wa Simba, Mfaransa, Hubert Velud, anatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa Jumamosi, kikosi cha timu hiyo kimejipanga kuivaa Singida United kwa tahadhari katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alisema kuwa kikosi chake kimejiandaa vizuri kuwakabili wageni hao, lakini akieleza kwamba mchezo huo hautakuwa mwepesi kwa timu zote mbili.

"Tumejiandaa na tumejipanga vizuri kwa ajili ya kucheza na Singida United, ni timu nzuri na yenye wachezaji wanaojua kupambana, Simba pia inajua inachohitaji katika mchezo huo."

Kikosi cha Simba ambacho kiliweka kambi yake Morogoro, kilitarajia kurejea Dar es Salaam jana jioni, tayari kuwavaa Singida United inayonolewa na Mholanzi, Hans van der Pluijm.

Velud anatua nchini kurithi mikoba iliyoachwa na Mcameroon, Joseph Omog, ambaye aliachana na Wekundu wa Msimbazi baada ya timu hiyo kutolewa na kuvuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa Velud (58), atatua nchini pamoja na wasaidizi wake wanne na pia watashirikiana na Mrundi, Djuma.

"Kocha mpya atawasili nchini Jumamosi, lakini bado kuna baadhi ya mambo hayajafanyiwa uamuzi wa mwisho, pande zote mbili ziko kwenye majadiliano, mchakato huu anaujua Salim (Abdallah-Kaimu Rais) na Mo (Mohammed Dewji," kilisema chanzo chetu.

Hata hivyo, Kaimu Rais, Salim, hakutaka kusema lolote kuhusiana na mchakato pamoja na ujio wa kocha huyo mpya ambaye ataiongoza timu pia kuelekea kwenye mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho mapema mwezi ujao.

Mechi nyingine ya Ligi Kuu itakayochezwa leo itakuwa ni kati ya Majimaji dhidi ya mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC ambayo itafanyika kuanzia saa 8:00 mchana.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.