Bongo Fc


Okwi, chirwa moto bado mdogo

Wachezaji Emmanuel Okwi na Obrey Chirwa wanashindana kufunga ndani ya ligi, lakini ushindani wao bado haujawa na maana sana kwa kuwa mpaka mzunguko wa kwanza unamalizika, idadi ya mabao yaliyofungwa kwenye ligi ni ndogo ikilinganishwa na misimu miwili iliyopita.

Mshambuliaji wa Simba, Okwi amefunga mabao 12, akifutiwa na Chirwa wa Yanga, John Bocco (Simba), Habib Kyombo (Mbao) na Mohammed Rashid (Prisons) kila mmoja akifunga mabao saba hadi sasa lakini mabao yao hayajafanya mzunguko wa kwanza wa msimu huu kuwa juu zaidi.

Tofauti na misimu miwili iliyopita, msimu wa 2015/2016 jumla ya mabao yaliyofungwa kwenye mzunguko wa kwanza yalikuwa ni 251, msimu uliofuata wa 2016/2017 mabao yaliyofungwa kwenye mzunguko wa kwanza yalikuwa ni 241 wakati msimu huu unaoendelea, umeshuhudiwa ukiwa na mabao machache zaidi kwenye mzunguko wa kwanza ambayo ni 207.

Yanga msimu uliopita ilifunga jumla ya mabao 57 katika ligi nzima ambayo yaliisaidia kuipa ubingwa mbele ya Simba iliyolingana nayo kwa pointi, ina kazi kubwa ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwenye mzunguko wa pili ili isiigharimu kutokana na rekodi mbaya ya ufungaji iliyoweka kwenye mzunguko wa kwanza.

Hadi mzunguko wa kwanza msimu huu unamalizika mwishoni mwa wiki iliyopita, Yanga ilikuwa imefunga mabao 20 tu tofauti na msimu uliopita ambapo ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na mabao 31. Ukiondoa Yanga, safu nyingine za ushambuliaji ambazo zimetepeta zaidi kwenye mzunguko wa kwanza msimu huu kulinganisha na msimu uliopita ni Azam FC, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Ndanda FC, Stand United na Ruvu Shooting.

Katika msimu uliopita, Azam FC ilimaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na mabao 21 na sasa imefunga 14, Kagera ilifunga mabao 16 na msimu huu imefunga saba, Mtibwa Sugar ilifunga jumla ya mabao 19 kwenye mzunguko wa kwanza wakati msimu huu imefunga mabao 11.

Ndanda ilifunga mabao 13 na sasa imeziona nyavu za wapinzani mara tisa, Stand ilifunga mabao 15 na msimu huu imefunga mabao matano wakati Ruvu Shooting ilifunga mabao 14 na sasa hivi imefunga mabao tisa.

Wakati timu nyingine zikionesha kutetereka kwenye safu ya ushambuliaji msimu huu, Simba imeimarika zaidi. Msimu huu Simba imefunga mabao 35 hadi mzunguko wa kwanza ulipokamilika wakati msimu uliopita timu hiyo ilikuwa imefunga mabao 26 tu katika mzunguko wa kwanza.

Kocha Msaidizi wa Azam, Iddi Cheche alisema ligi ni ngumu na kila timu imejiandaa vizuri na ndio maana inakuwa vigumu kupata ushindi wa mabao mengi.

“Sisi kama Azam FC tuna malengo yetu tumejiwekea na ili yatimie ni lazima tupate ushindi kwenye mechi. Huo ndio mkakati wetu wa kwanza halafu baada ya hapo ndio hayo mambo mengine yatafuata,” alisema Cheche.

Kocha wa Msaidizi wa Simba Mrundi, Masoud Djuma alisema ukame wa mabao unachangiwa na ubora wa timu zinazoshiriki msimu huu.

“Maisha yanabadilika, hivyo usitegemee kuona timu ilivyocheza jana, ndio ije kucheza leo au kesho na hili ndilo ninaloliona kwenye ligi. Timu zinaimarika siku hadi siku na ndio maana ligi inakuwa ngumu,” alisema Djuma.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.