Bongo Fc


Orodha ya wakali wa kusambaza mipira uwanjani

Na: Omary Ramsey

Mesut Ozil amebamba bonge la mkataba huko Arsenal. Mkataba wake mpya wa miaka mitatu aliosaini Emirates unamfanya awe analipwa Pauni 300,000 kwa wiki. Ni pesa nyingi.

Lakini kwa taarifa yako tu, Arsenal hawakuwa wajinga kumpa Mjerumani huyo dili la pesa nyingi hivyo, bali walivutiwa na mchango wake na kwa data zilizokusanywa hadi mwanzoni mwa Februari, Ozil ndiye kiboko ya wote kwa kutengeneza nafasi za mashambulizi tangu alipotua Arsenal mwaka 2013.

Kwa data zake, anawafunika mastaa kibao tu unaowafahamu wewe wanatisha wanapokuwa ndani ya uwanja. Hizi data zilizokusanywa hadi Februari 2, 2018 na hazihusu mipira iliyokufa.

7. Alexis Sanchez – nafasi 46

Kwa sasa anavaa jezi za Manchester United baada ya kujiunga kwenye dirisha la mwezi uliopita akitokea Arsenal. Kwa data zilizokusanywa hadi Februari, Sanchez alikuwa amecheza mechi 20 kwenye Ligi Kuu England na kufanikiwa kutengeneza mashambulizi 46 yanayomfanya aingie kwenye orodha ya wababe wa kupika mashambulizi.

Staa mwingine wa Ulaya aliyesababisha mashambulizi kama hayo ni Florian Thauvin wa Marseille, ambaye amecheza mechi 23 kwenye Ligue 1.

6. Kevin De Bruyne – nafasi 47

Staa wa Kibelgiji, De Bruyne msimu huu anacheza soka la ndoto zake huko Manchester City. Kiwango chake kimeifanya timu hiyo inayonolewa na Pep Guardiola kutamba kwenye ligi na kuongoza msimamo kwa tofauti ya pointi 13 dhidi ya wapinzani wao Manchester United wanaoshika nafasi ya pili.

Makali ya De Bruyne ni hatari baada ya kutengeneza mashambulizi 47 katika mechi 25 alizocheza kwenye Ligi Kuu England.

5. Dele Alli – nafasi 48

Staa wa Kiingereza, Dele Alli haonekani kuwa na ubora mkubwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu, lakini jambo hilo halijamfanya ashindwe kutimiza wajibu wake kwenye kikosi cha Tottenham. Pengine kinachokosekana kwa Dele Alli ni mabao tu, lakini katika mechi 24 alizocheza kwenye ligi akiwa na Spurs msimu huu, ametengeneza mashambulizi 48. Mchezaji mwingine aliyetengeneza nafasi kazi hizo ni Ivan Perisic wa Inter Milan huko kwenye Serie A baada ya kucheza mechi 22.

4. Neymar – nafasi 50

Mwanasoka ghali kabisa duniani kwa sasa baada ya saini yake kuigharimu Paris Saint-Germain, Pauni 198 milioni ilipomnasa kutoka Barcelona. Kutokana na data zilizokusanywa hadi kufikia Februari 2, Neymar alikuwa amecheza mechi 16 kwenye Ligue 1 msimu huu na kufanikiwa kutengeneza nafasi za mashambulizi 50.

Neymar amekuwa staa mkubwa kwelikweli huko katika kikosi cha PSG, lakini siku za karibuni jina lake limekuwa likihusishwa na Real Madrid.

3. Lionel Messi – nafasi 51

Barcelona kwa sasa imecheza mechi 22 kwenye La Liga, lakini kwa rekodi zilizokusanywa kwenye mechi 20 za ligi hiyo, supastaa wa timu hiyo, Lionel Messi alikuwa ametengeneza nafasi za mashambulizi 51. Messi hakuna shaka juu ya uwezo wa soka lake, lakini kwenye timu mambo haya, amezidiwa na Ozil.

Ubora wa Messi unadaiwa kuwa kizunguzungu kwa Chelsea ambao italazimika kumkabili Muargentina huyo kwenye mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

2. Lorenzo Insigne – nafasi 56

Katika msimu huu, Napoli inajivunia kuwa na huduma bora kabisa kutoka kwa staa wake Lorenzo Insigne. Huduma yake haina shaka katika mechi 21 alizocheza kwenye Serie A, staa huyo ametengeneza nafasi za mashambuliaji 56.

Ndiyo maana huduma yake inasakwa. Lorenzo ni mmoja kati ya wachezaji walio kwenye ubora mkubwa kwenye Ligi kuu Italia na kutajwa na vigogo kibao wa timu nyingine za Ulaya zikitazama uwezekano wa kuinasa huduma yake.

1. Mesut Ozil – nafasi 60

Unaweza kumwita mfalme wa kutengeneza mashambulizi. Kwenye Ligi Kuu England msimu huu, mechi zake 20 alizocheza, Ozil ametengeneza nafasi 60 za mashambuliazi na hivyo kuifanya safu ya ushambuliaji ya Arsenal kuwa hai na tishio kwa mabeki wa timu pinzani.

Amefunika Ulaya nzima. Mkataba wake aliosaini hivi karibuni wa kumfanya aendelee kubaki Emirates umemfanya awe na pesa za kutosha kutokana na kupokea Pauni 300,000 kila wiki.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.