Bongo Fc


Noma sana!! mwamuzi simba, azam abadilishwa, tff yaanika sababu hii..

Yanga, leo Jumanne inashuka Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuikaribisha Njombe Mji, lakini gumzo kubwa ni kitendo cha mwamuzi wa FIFA aliyekuwa azichezeshe Simba na Azam kesho Jumatano kubadilishwa ghafla saa chache kabla timu hizo hazijavaana.

Mwamuzi huyo, Jonesia Rukyaa, aliyekuwa amepangwa kulichezesha pambano hilo litakalopigwa Uwanja wa Taifa, ameondolewa na nafasi yake kupewa Emmanuel Mwandembwa.

Bodi ya Ligi ikishirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), vimeamua kumkabidhi Mwandembwa mchezo huo unaozikutanisha klabu zinazofukuzana kileleni mwa msimamo, Simba yenye alama 38 na Azam iliyo na alama 33.

Habari kutoka ndani ya TFF zinasema Mwandembwa atasaidiwa na waamuzi wa pembeni, Sudi Lila wa Dar es Salaam na Mohammed Mkono kutoka Tanga. Awali ratiba ya waamuzi ilikuwa ikionyesha Jonesia angesaidiwa na Lila na Helen Mduma wote wa Dar.

Hata hivyo imeelezwa sababu kubwa iliyotajwa ya kubadilishwa kwa Rukyaa ni kwa vile anajiandaa kuchezesha mechi za kimataifa, hivyo wameamua kumwondoa ili apate muda wa kutosha kujiandaa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Waamuzi Tanzania (Frat), Oden Mbaga, alisema: “Ni kweli kuna mabadiliko na sasa Mwandembwa atachukua nafasi ya Jonesia, pia wale wa pembeni wamebadilishwa.”

MECHI YENYEWE

Azam itaingia kwenye mechi ya kesho kwa tahadhari kubwa kutokana na kasi ya ushambuliaji ya Simba iliyofunga mabao 13 katika mechi nne za mwisho ilizocheza.

Timu hizo zinakutana mwezi mmoja tu tangu zilipokutana kwenye Kombe la Mapinduzi ambapo Azam ilishinda bao 1-0 na katika mechi yao ya duru la kwanza iliyochezwa Uwanja wa Azam Complex, timu hizo zilishindwa kufungana.

Kocha Msaidizi wa Simba, Mrundi Masudi Djuma, ametangaza silaha tatu zakuwamaliza Azam ambao wiki moja iliyopita walifungwa mabao 2-1 na Yanga iliyopo nafasi ya tatu Ligi Kuu.

Djuma alisema makali ya safu yake ya ushambuliaji ambayo inaongozwa na John Bocco aliyefunga magoli tisa, Emmanuel Okwi mwenye 12, pamoja na Shiza Kichuya aliyefunga mara sita ndiyo inawapa kiburi cha kuamini kuwa Wanalambalamba hao hawawezi kufua dafu mbele yao.

“Tumecheza mechi tano, tumefunga magoli 15. Inaonyesha kuwa tuna timu nzuri lakini safu yetu ya ushambuliaji imekuwa kali na nina imani tutaweza kufunga kwenye mechi ijayo dhidi ya Azam,” alisema.

Kocha Msaidizi wa Azam, Iddi Cheche, alisema wanaiheshimu Simba na mastaa wao wanaotamba sasa, lakini wataingia kwenye mchezo huo kushindana.

“Tunamfahamu vizuri Bocco, alikuwa mchezaji wetu hapa na sasa anafanya vizuri na Simba. Tunafahamu nguvu na udhaifu wake, tutaweza kumdhibiti,” alisema Cheche.

Wakati huo huo, Meneja wa Simba, Richard Robart, ‘Mwana’ alisema staa wao Emmanuel Okwi aliyeumia kwenye mechi ya juzi Jumapili dhidi ya Ruvu Shooting anaendelea vizuri na yupo kambini.

“Okwi aliumia shingoni, lakini tuliamua kumtoa ili kupata matibabu zaidi kuliko angeendelea kucheza. Amepata matibabu na afya yake inaendelea vizuri,” alisema.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.