Bongo Fc


simba, azam ngoma hailali

Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba leo watakuwa nyumbani kujaribu kuendeleza kasi yao ya ushindi itakapowakaribisha Azam FC na tayari makocha wa timu hizo wameshusha tambo zao, kila mmoja akijinasibu kushinda.

Kocha msaidizi wa Simba, Mrundi Masoud Djuma, aliiambia BongoFC jana, kuwa wanaiheshimu Azam kwa kuwa ni moja ya timu bora na ngumu kwenye ligi, lakini anajivunia kasi ya timu yake na utimilifu wa wachezaji wake.

"Itakuwa moja ya mechi nzuri..., lengo letu ni ushindi na tunaujua ubora wa wapinzani wetu upo wapi, lakini nakiamini zaidi kikosi changu," alisema Djuma.

Alisema mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi ambaye alipigwa kiwiko na kulazimika kutoka nje kwenye mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting yupo katika ari nzuri.

"Ushindi utatuweka kwenye morali ya juu zaidi kuelekea kwenye mchezo wetu wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho wiki hii," alisema Djuma.

Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, itaumana na klabu ya Gendarmarie ya Djibouti Jumapili kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kwa upande wake, kocha msaidizi wa Azam, Iddi Cheche, alisema kuwa watapambana kujaribu kupunguza pengo la pointi dhidi ya vinara hao.

"Bado tunautaka ubingwa, Simba wametuzidi kwa pointi tano, tunaamini kama tukifanikiwa kushinda na zikabaki pointi mbili tutakuwa tumekoleza kasi yetu ya ubingwa," alisema Cheche.

"Huu ni mpira na katika mpira lolote linaweza kutokea, hivyo hatuiogopi Simba wala timu yoyote kwenye ligi," aliongezea kusema Cheche.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.