Bongo Fc


Kuelekea simba vs azam fc, huu ndiyo udhaifu wa razaq abarola (kipa azam fc)

Na: Baraka Mbolembole

Kuelekea mchezo wake wa 17 katika ligi kuu ya Tanzania Bara Jumatano hii, hakika golikipa wa Azam FC, Mghana, Razaq Abarola ameonyesha kuwa anaweza kuwa chaguo sahihi kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Aishi Manula aliyejiunga na Simba SC. Akiwa tayari amekwishacheza michezo 16, kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 ameonekana kuendana na soka la Tanzania ikiwa ni miezi saba tu tangu aliposajiliwa kutoka kwao Ghana.

Kiwango chake katika mchezo vs Simba SC mwezi Septemba kilionyesha ni kweli golikipa huyo alikuwa sehemu ya timu ya Taifa ya vijana ya Ghana. Abarola amekuwa akijipanga vizuri golini, amekuwa mtulivu na mchezaji ambaye anaitazama timu yote inavyocheza na kusahihisha pale kwenye makosa.

Goli la kwanza kwake kuruhusu ilikuwa dhidi ya Singida United katika mchezo wa raundi ya tano katika uwanja wa Jamhuri, Dodoma na hadi kufikia wikendi iliyopita kipa huyo alikuwa amecheza michezo kumi pasipo kuruhusu goli katika mechi 17 zilizopita huku goli lake la mwisho kufungwa likiwa lile vs Ndanda FC Jumapili iliyopita wakati Azam FC iliposhinda 3-1 katika uwanja wa Chamanzi.

Goli la ‘free kick’ alilofungwa na Kelvin Sabato ‘Kiduku’

Abarola aliruhusu goli la pili katika mchezo wa pili mfululizo wakati Azam FC ilipolazimisha sare ya kufungana 1-1 na Mwadui FC katika dimba la Mwadui Complex katika wiki ya sita. Akacheza michezo mingine minne mfululizo na kutimiza jumla ya michezo nane pasipo kuruhusu goli. Hii ilikuwa baada ya ligi kufika raundi ya kumi hivyo tayari alikuwa amejidhihirisha kuwa anaweza kuisaidia timu yake kama watafunga magoli kwa timu pinzani.

Mchezo wake wa 11 akaruhusu goli la tatu wakati Azam FC ilipolazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Mtibwa Sugar FC katika uwanja wa Azam Complex. Azam ikiwa mbele 1-0, Mtibwa ilipata mkwaju wa adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la hatari, na mshambulizi aliyeingia akitokea benchi, Kelvin Sabato ‘Kiduku’ akafunga kwa free kick moja ‘maridadi’ sana ambayo kipa huyo wala hakuangaika kuufuata mpira ule.

Sabato alipitisha mpira katika ukuta wa wachezaji wa Azam FC na kwa vile mpira huwa na kasi kuliko mchezaji, Abarola alishindwa kutoka eneo alilokuwepo ili kuuokoa. Goli hili lilinipa nafasi ya kumfuatilia zaidi Abarola na nilichokuja kugundua ni kwamba kipa huyo bado si mwepesi na mikwaju ya mbali inampa shida kuizuia.

Udhaifu wake

Licha ya kujipanga vizuri golini na kuwasisitiza mara kadhaa walinzi wake, Abarola si mwepesi wa kujituma yeye mwenyewe. Goli lake la nne kuruhusu lilikuwa dhaifu mno. Licha ya kwanza kuna makipa waliwahi kufungwa kwa mipira ya kona ya moja kwa moja-Juma Kaseja na Ivo Mapunda waliwahi kufungwa hivyo na Amandus Nesta. Shiza Kichuya pia aliifunga Yanga kwa goli la kona ya moja kwa moja msimu uliopita, lakini bao la Marcel Bonaventure vs Abarola wakati Azam FC ilipolazimishwa sare ya 1-1 na Majimaji FC wiki mbili zilizopita lilitoa picha nyingine kuhusu kipa huyo wa mabingwa wa Mapinduzi Cup.

Marcel awali alijaribu kupiga kona ya moja kwa moja lakini kipimo chake kilikuwa kikubwa, ila kwa vile aliona kipa huyo anasogea sana-mbele karibia na mlingoti wa kwanza upande anaopigia mpira, akakadiria kipimo na kuongeza nguvu katika upigaji wake wa mpira ndiyo maana mara ya pili alipopiga alifunga kirahisi. A

barola ameonyesha si mzuri wa kucheza krosi za juu hasa zile zinapigwa na mguu wa kushoto kutokea upande wa kulia kwake au zile zinazopigwa na mguu wa kulia kutokea upande wa kushoto. Ni kipa mzuri na uwezo wa kocha wake Idd Abubakary unaweza kumfanya aondoe kasoro hizo ndogondogo ambazo zinaweza kuiangusha timu yake.

Katika mchezo wa raundi ya 15, Abarola aliruhusu magoli mawili ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu aliposajiliwa Azam FC. Ilikuwa ni katika mchezo ambao Azam FC ilipoteza 1-2 nyumbani dhidi ya mabingwa watetezi Yanga SC. Goli la kwanza ambalo Yanga walisawazisha kupitia kwa Obrey Chirwa mlinda mlango huyo alionyesha udhaifu mwingine katika uchezaji wa ‘mtu kwa mtu’ kwani alishindwa kuwapanga walinzi wake, ila pia wakati anatoka golini ili kuuwahi mpira uliokuwa ’50/50’ kati yake na Chirwa hakuwa amefanya maamuzi. Idd anaweza kutazama vizuri baadhi ya marudio ya michezo ambayo Razaq aliruhusu magoli na kumsaidia kipa huyo na si kuendelea kuamini kuwa ni bora wakati kuna makosa rahisi-rahisi amekuwa akiyafanya.

Timu dhaifu kiufungaji haziwezi kumfunga

Singida, Mwadui, Mtibwa, Yanga na Ndanda ndio timu pekee zilizomfunga Abarola hadi sasa katika ligi. Hii inaonyesha kuwa kuna timu kumi ambazo zimeshindwa kumfunga Abarola. Alicheza michezo minne mfululizo ya mwanzo wa msimu pasipo kuruhusu goli-vs Ndanda, Simba, Lipuli FC na Kagera Sugar FC. Hakuruhusu pia bao katika michezo mingine minne mfululizo vs Mbao FC, Mbeya City FC, Ruvu Shooting, Njombe Mji FC pia hakuruhusu goli vs Stand United na Tanzania Prisons.

Ukitazama uwezo wa kiufungaji wa timu hizo kumi zisizomfunga Abarola utagundua kuwa ni Simba pekee ambayo labda inaweza kuonekana ina wafungaji hatari lakini bahati njema kwa kipa huyo ni kwamba alikutana na Simba ambayo haikuwa na Okwi wala John Bocco kwa pamoja msimu.

Hii inamaanisha kuwa kama timu isiyo na makali katika mashambulizi itakutana na Abarola haitakuwa rahisi kwake kuruhusu goli, lakini kama timu itajaribu mara kwa mara kupiga mpira golini kwake basi itafunga kwa maana kipa huyo licha ya ubora wake katika baadhi ya maeneo ni ‘nyanya’ katika mikwaju ya mbali, faulo na si mzuri katika kutokea.

Kucheza vs Simba ikiwa imefunga magoli 38-magoli 31 zaidi ya yale wakati alipocheza nao kwa mara ya kwanza itakuwa mtihani mwingine kwa Abarola Jumatano hii. Ni wakati wake wa kusahihisha na kudhihirisha kuwa yeye ni bora-na ubora hupimwa zaidi katika michezo mikubwa.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.