Bongo Fc


Conte atapona? west brom imefukuzisha makocha kibao

Si umesikia Antonio Conte anapumulia mashine huko Stamford Bridge?

Asikwambie mtu, kibarua cha Mtaliano huyo kuwa kocha wa Chelsea kipo kwenye wasiwasi mkubwa na bahati mbaya, timu inayofuata anayokwenda kukumbana ina mkosi wa kufukuzisha makocha.

Chelsea itakipiga na West Brom kwenye Ligi Kuu England Jumatatu ijayo huko Stamford Bridge na Albion ina nuksi ya kufukuzisha makocha, kuna makocha kibao wametimuliwa na timu zao baada ya kucheza na timu hiyo.

Cheki orodha ya makocha waliofukuzwa kazi baada tu ya kucheza na West Brom.

(01) Shakespeare – Leicester City

Kocha Craig Shakespeare ni mmoja kati ya watu waliokumbana na gundu la kufukuzwa kazi baada ya kucheza na West Brom, Oktoba 2017 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 tu uwanjani King Power. Shakespeare alikuwa kocha wa Leicester City kwa wakati huo.

(02) Chris Hughton – Norwich City

Aprili 2014, Chris Hughton alifutwa kazi huko Norwich City baada ya kuchapwa 1-0 na West Brom iliyokuwa chini ya Kocha Pepe Mel kwa wakati huo.

Kichapo hicho kilikuwa na madhara makubwa kwa Norwich na kushuka daraja baada ya mechi nne zilizofuatia, lakini Hughton hakupona.

(03) Paolo Di Canio – Sunderland

Di Canio ni kocha mwingine aliyekumbana na nuksi ya West Brom. Baada ya kuchukua mikoba ya kuinoa Sunderland mwaka 2013, ilipokuwa kwenye hali mbaya ya kushuka daraja, Di Canio aliisaidia haikushuka, lakini msimu uliofuatia ilipofika Septemba 2013 tu, ukawa mwisho wake kwenye kikosi cha Sunderland baada ya kuchapwa mabao 3-0 na West Brom.

(04) Roberto Mancini – Man City

Mtaliano Roberto Mancini alionekana kuwa ni kocha mwenye mafanikio kwenye kikosi cha Manchester City baada ya kuisaidia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England uliokuwa wa kwanza kwa upande kwake baada ya kusubiri kwa miaka kibao.

Lakini, kibarua chake klabuni hapo kilifika tamati baada ya mechi yake dhidi ya West Brom kwenye ligi. Man City ilishinda 1-0 kwenye mechi hiyo, lakini gundu likamwaandama Mancini na alipokwenda kupoteza tu na Wigan kwenye fainali ya Kombe la FA, safari ikamhusu.

(05) Roberto Di Matteo – Chelsea

Mtaliano mwingine aliyewahi kukumbana na nuksi za West Brom. Di Matteo alitua Chelsea kuchukua mikoba ya Andre Villas-Boas na aliisaidia kwenda kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini mechi yake ya mwisho Chelsea ilikuwa kwenye kipigo cha 3-0 kutoka kwa Juventus kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliofuatia. Lakini, Juve ilikuwa kama inahitimisha tu, gundu la Di Matteo lilianzia kwa West Brom wakati ilipochapwa 2-1 kwenye Ligi Kuu England na hivyo ndiyo ilikuwa mechi yake ya mwisho kwenye ligi hiyo.

(06) Andre Villas-Boas – Chelsea

Mreno AVB alipoteza kibarua chake huko Chelsea baada ya kuinoa timu hiyo kwa miezi tisa tu. Kibarua chake kiliota mbawa baada ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa West Brom huko The Hawthorns, ambao uliifanya iwe imeshinda mechi tatu tu za Ligi Kuu England kati ya 12.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.