Bongo Fc


Niyonzima kwenda india kwa matibabu zaidi

Ili kuhakikisha anapona haraka na kuongeza nguvu katika kikosi chao, mabosi wa Simba wamesema kuwa kiungo wao wa kimataifa Mnyarwanda, Haruna "Fabregas" Niyonzima, ataondoka nchini muda wowote kuelekea India kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi, imeelezwa.

Niyonzima aliyetua Simba akitokea Yanga amekuwa nje ya timu tangu mwaka jana akiuguza maumivu ya goti na safari yake hiyo ya India inalenga kwenda kufanyiwa upasuaji.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa wanaamini baada ya kwenda kupata matibabu, Niyonzima atarejea kwenye kikosi na hatimaye kuongeza nguvu katika harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

"Haruna Niyonzima anatarajiwa kusafiri katika siku mbili hizi kwenda India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji mdogo kwenye mguu, haitachukua zaidi ya wiki mbili atakuwa amerejea uwanjani," alisema Manara.

Aliongeza kuwa wachezaji wengine wa timu hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri Matokeo ya SportPesa waliokuwa majeruhi ambao ni kipa Saidi Mohammed na beki wa kati, Salim Mbonde, nao wameshaanza kujifua pamoja na wenzao na kilichobaki ni uamuzi wa kocha kuanza kuwatumia nyota hao.

Wakati huo huo Manara alisema maandalizi ya mechi yao ya raundi ya awali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa yako katika hatua za mwisho na kuongeza kuwa kiingilio cha juu ni Sh. 30,000 na cha chini ni Sh. 5,000.

"Natoa wito kwa mashabiki wa Simba watakaoenda uwanjani katika mechi ya Yanga siku ya Jumamosi wasizomee, tuzomeane kwenye ligi ya nyumbani, sisi sote ni Watanzania na tunaiwakilisha nchi," alisema Manara.

Yanga yenyewe inatarajiwa kuwakaribisha St. Louis FC kutoka Shelisheli katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakati vinara wa ligi nchini, Simba wakiwapokea Gendarmarie Nationale ya Djibouti kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho, timu hizo zitarudiana kati ya Februari 20 na 21 mwaka huu.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.