Bongo Fc


Hii hapa sababu magufuli, rais fifa kukutana

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, anatarajiwa kuwa mmoja wa viongozi watakaokutana na ujumbe wa Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Gianni Infantino, ambao utawasili nchini Februari 20, mwaka huu, imeelezwa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, alisema kuwa utaratibu wa viongozi hao wawili kukutana unaandalia lengo likiwa ni kurahisisha utekelezaji wa programu mbalimbali za maendeleo zitakazopitishwa.

Waziri Mwakyembe alisema kuwa serikali imefurahishwa na uamuzi wa Fifa kuuleta mkutano wake nchini na wanaahidi kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuwapokea vyema wajumbe wote watakaokuja kuhudhuria mkutano huo.

"Nawaomba tuupokee vizuri ugeni, mkutano huu una uwezo wa kubadilisha sura ya Tanzania, waliyofanya Rwanda ni makubwa sana, tunataka kuona baada ya kuondoka wanafanya mambo yatakayoleta maendeleo, tunajua sera za Rais wa Fifa, anasafisha safu ya Fifa, hataki upuuzi, anataka mambo yaliyonyooka kama ambavyo Rais wa nchi yetu (Magufuli) anavyofanya," alisema Mwakyembe.

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia, alisema kuwa mkutano huo utahusisha viongozi wa nchi 21 ambazo ni pamoja na Tanzania.

Alitaja baadhi ya mambo yatakayojadiliwa ni mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao na changamoto zake na jinsi ya matumizi ya fedha za maendeleo wanazopata kutoka Fifa ambazo wataomba ziongezeke.

"Awali ulikuwa uwe na wajumbe kutoka nchi 19, lakini sasa zitakuwa 21 baada ya Uganda na Malawi kuomba kuja ikiwa ni pamoja na wenyeji Tanzania," alisema Karia.

Aliongeza kuwa viongozi hao wa Fifa watakuja nchini wakitokea Nigeria ambako pia walikuwa na mkutano mwingine kwa lengo la kupanga ajenda za mkutano mkuu ujao wa shirikisho hilo linalosimamia soka duniani.


Facebook Twitter

Match Highlights                  

Newsletter                           

Subscribe to our newsletter for good news, sent out every time we post.